Lewa Marathon: Baaru ashindikana, Lepekana hoi

Saturday June 30 2018

 

Isiolo, Kenya. Mwanariadha Philemon Baaru, amefanikiwa kutetea ubingwa wa mbio za hisani za Lewa Marathon, Kilomita 42, kwa mara ya sita mfululizo, katika makala ya 19 ya mbio hizo, zilizofanyika leo katika hifadhi ya wanyama ya Lewa, mjini Isiolo, kaunti ya Meru.

Baaru, mwenye umri wa miaka 36, alitumia muda wa saa 2:5:39, dakika moja nyuma ya muda aliyoweka katika mbio za mwaka jana (2:19:26), kushinda mbio hizo zinazofanyika kia mwaka.

Akionekana kuwa na nguvu isiyomithilika, Baaru aliwashangaza watazamaji, baada ya kumuacha mshindi wa pili, Peter Wahome, aliyevuka utepe, akitumia muda wa saa 2:22:23, kwa zaidi ya mita 200, zikiwa zimesalia kilomita 10 mbio zimalizike. Nafasi ya tatu ilienda kwa Muturi Silas (2:23:23).

Kwa upande wa wanawake, mbio za kilomita 42, mshindi alikuwa ni Jane Ngima, aliyevuka utepe, akitumia muda wa saa 2:51:36. Esther Macharia alimaliza katika nafasi ya pili, akitumia muda wa saa 2:53:41 huku nafasi ya tatu ikienda kwa Mary Mwaniki 3:29:31.

Akizungumza na Mwanaspoti Digital, baada ya kumaliza mbio hizo, Baaru hakusita kufichua siri za mafanikio yake katika makala sita mfululizo huku akishukuru hali ya hewa kuwa nzuri tofauti na miaka ya nyuma.

"Mbio hazikuwa ngumu sana, japo mwaka huu kulikuwa na uhindani mkubwa sana tofauti na makala zilizopita. Siri ya mafanikio ni familia yangu, hasa mwanangu, amekuwa mstari wa mbele kunipa sapoti, kingine ni kula vizuri, mazoezi na kumjua Mungu,” alisema Baaru

Advertisement

Tangu mwaka 2000, ambapo mbio za kwanza zilizpofanyika, Lewa Marathon, imekuwa ikifahamika kote duniani kutokana na ugumu wake, hasa hali ya hewa isiyotabirika, njia zisizoeleweka na washiriki wakubwa katika medani ya riadha.

Baadhi ya majina makubwa kuwahi kushiriki mbio hizi ni mshindi wa fedha katika michezo ya Olimpiki, mwaka 2004, Catherine Ndereba na Rais wa Kamati ya Olimpiki ya Kenya (NOCK), Paul Tergat.

 

Advertisement