Diamond League: Chepkoech aweka rekodi ya Dunia, mita 3000

Saturday July 21 2018

 

By Fadhili Athumani

Nairobi. Mshindi wa medali ya fedha katika michezo ya Jumuiya ya Madola, Beatrice Chepkoech jioni ya jana Ijumaa, Julai 20, aliweka rekodi mpya ya Dunia, katika mashindano ya IAAF Diamond League yanayofanyika mjini Monaco, Ufaransa, akitumia muda wa dakika 8:44.32 kumaliza mbio za mita 3000.
Chepkoech alikuwa kivutio katika mbio hizo, baada ya kuwaacha wenzake kwa umbali wa mita 90, zikiwa zimesalia mita 1000 kufikia utepe, na kufanikiwa kutwaa ushindi wake wa tatu katika makala ya mbio za Diamond League huku akivunjilia mbali rekodi ya dakika 8:52.78 iliyowekwa na Mkenya mwenzake, Ruth Jebet, Jijini Paris miaka miwili iliyopita.
Dalili ya ushindi wa Chepkoech, ilionekana mapema tu, baada ya mwanadada huyo kutumia sekunde 16 kujitenga kutoka katika kundi la wanariadha wenzake. Iliofika mita 2000, tayari ilikuwa wazi kuwa medali ya dhahabu imeenda Kenya, na kilichobaki ni kufukuzia rekodi.
Chepkoech, ambaye alimaliza katika nafasi ya nne, kwenye michezo ya Olimpiki mwaka 2016 na mashindano ya ubingwa wa Dunia 2017, alikuwa mshikilizi wa muda bora kwenye michuano ya Diamond League ya Paris, akitumia muda wa dakika 8:59.36.
Katika mbio za jana, mshindi wa fedha katika mbio za ubingwa wa dunia, Mmarekani Courtney Frerichs, alimaliza wa pili, akitumia muda wa dakika 9:00.85 kuweka rekodi ya Bara Amerika Kaskazini huku nafasi  ya tatu ikienda kwa Mkenya Hyvin Kiyeng, ambaye ni bingwa wa Dunia, aliyevuka utepe ndani ya dakika 9:04.41.

Advertisement