Zimbabwe yapata pigo Kutinyu aumia kuikosa AFCON

Muktasari:

Zimbabwe ipo Kundi A pamoja na Misri, DR Congo, na Uganda, na watacheza mechi ya ufunguzi dhidi ya Misri kesho Juni 21.

Cairo, Misri. Kiungo wa Zimbabwe, Tafadzwa Kutinyu ameondolewa katika kikosi cha nchi hiyo kitakachoshiriki Afcon 2019 baada ya kupata majeraha ya misuli siku tatu kabla ya mechi yao ya ufunguzi dhiid ya Misri.

Zimbabwe ‘The Worriers’ ipo Kundi A pamoja na Misri, DR Congo, na Uganda, na watacheza mechi ya ufunguzi dhidi ya Misri kesho Juni 21.

Siku moja kabla ya kuanza kwa mashindano Zimbabwe imepata pigo kubwa kutokana na kuumia kwa kiungo Tafadzwa Kutinyu hatoweza kucheza mashindano hayo.

Kutinyu mwenye miaka 24, ndiyo kwanza amejiunga na mabingwa wa Guinea, Horoya AC mwezi uliopita akitokea Azam FC, alifanyiwa vipimo jana Jumatano na kuonyesha kwamba hataweza kupona katika muda wa mashindano ya AFCON.

Kocha wa Zimbabwe, Sunday Chidzambwa amemwita kiungo wa FC Platinum, Lawrence Mhlanga kuziba pengo la Kutinyu aliyeondolewa.

Meneja wa timu hiyo Wellington Mpandare alisema: “Ni hudhuni kubwa kutangaza kuwa Kutinyu hatoweza kucheza mashindano haya kwa sababu ya kuumia katika mchezo wa kirafiki tuliocheza hapa.

“Ni pigo kwa sababu ni mchezaji muhimu kwetu kutokana na nafasi yake katika kikosi chetu.”