Zahera kumbe katumia Sh114 milioni Yanga, afichua madudu ya safari

Muktasari:

Leo kocha huyo kutoka DR Congo anaendelea kufunguka mambo mengi zaidi ikiwamo kiasi cha fedha anazodai kutumia akiwa ndani ya Yanga pale viongozi waliposhindwa kutimiza wajibu wao, huku akikanusha tuhuma kadhaa za kuwabeba Wakongo wenzake kikosini. Endelea naye...!

JANA Alhamisi tuliona namna Kocha Mwinyi Zahera akifunguka juu ya mambo kibao yaliyopo ndani ya mkasa wake wa kusitishiwa mkataba na Yanga na kuanika ishu nzima ya usajili wa klabu hiyo na anavyoshangaa kutimuliwa akidai ni kwa shinikizo la wanachama.

Leo kocha huyo kutoka DR Congo anaendelea kufunguka mambo mengi zaidi ikiwamo kiasi cha fedha anazodai kutumia akiwa ndani ya Yanga pale viongozi waliposhindwa kutimiza wajibu wao, huku akikanusha tuhuma kadhaa za kuwabeba Wakongo wenzake kikosini. Endelea naye...!

UONGOZI MPYA ULIPOINGIA

Zahera anafichua namna uongozi mpya ulivyoingia madarakani kulikuwa na mabadiliko gani? Msikie alivyojibu: “Hakuna kibaya tulikuwa tunaishi nao vizuri tunaongea na kukubaliana, ingawa kuna changamoto baadhi pia zilikuwepo ambazo zilikuwa zinaonyesha Yanga bado haijawa na muundo mzuri wa utawala. Unajua Yanga ni klabu kubwa kweli, hilo halipingiki lakini kuna mambo ambayo yanafanyika unaona kabisa yanashusha hadhi ya kuwa klabu kubwa na kongwe.

“Unajua kila mmoja anajua kwamba msimu uliopita Yanga haikuwa na maisha mazuri kila kitu kilikuwa hakina uhakika, lakini msimu huu akili za watu wengi wanadhani mambo yako vizuri kila kitu kipo sawa, ukija ndani mambo yako tofauti kuna changamoto nyingi.”

CHANGAMOTO ZA SAFARI

Kuhusu safari, anasema “unaweza kuangalia kuna wakati tulienda Botswana tukachukua ndege mpaka Afrika Kusini, tukitoka hapo tunachukua basi mpaka Botswana, ni safari ndefu ya masaa yasiyopungua sita wachezaji wanalalamika chakula, lakini ukiangalia hakuna kilichopangwa wakati wa kurudi, hivyo hapo inakulazimu wewe kama kocha utoe pesa uwanunulie wachezaji chakula, sasa kwa klabu kama Yanga hili ni tatizo.”

VIONGOZI WALIOTANGULIA

Anasemaje kuhusu viongozi waliotangulia? “Hilo ukiniuliza nitakuwa sina majibu, swali hilo ni bora uwaulize viongozi waliokuwa wanapanga hayo, mimi kama kocha nilikuwa sitaki kuona wachezaji wangu wanateseka.

“Hali hiyo pia ilitokea tulivyokwenda Zambia - tukienda kucheza na Zesco, kutoka hapa tunatumia ndege mpaka Lusaka baada ya hapo tunakuta mabadiliko tunatakiwa kutumia basi mpaka Ndola na ni safari ya masaa matano, sasa unajiuliza kwanini hatukuenda moja kwa moja mpaka Ndola na ndege? Huko nako wapo viongozi walitangulia wachezaji wanalalamika tena chakula, tunamuuliza meneja kama amepewa pesa ya chakula anasema hapana labda viongozi, ikabidi nimwambie dereva asimame sehemu wachezaji wale chakula, natoa pesa yangu wakati huo wale viongozi walishatangulia wote kule Ndola.

“Tulipofika Ndola matatizo tena hakuna uwanja wa mazoezi, kupata uwanja wa nyasi bandia kufanyia mazoezi nikauliza kukodi uwanja kwa mazoezi ni kiasi gani? Wakasema ni dola 200 (Sh456,000) kwa siku, nikalipa kwa siku mbili, sasa nikauliza sababu gani klabu inatuma watu kutangulia na hawana pesa? Kazi yao ni kufanya nini mpaka kocha anatoa pesa zake? Tulipokuwa huko tulifanya kikao kifupi humo ndani nikawauliza kazi yao ni ipi kama wao wapo na timu haina pesa?”

Anasema, “unaweza siku ukapata tatizo mchezaji anaanguka, au msaidizi wangu anapata shida tutamwacha afe kweli? Haya yote mambo madogomadogo yanaonyesha kwamba timu bado ina shida, nayasema haya ili watu wa Yanga waone vile timu yao inaendeshwa, naona kama mashabiki wanajua mambo ya viongozi yao yako mazuri wakati kuna mambo ya ajabu.”

KURUDISHIWA FEDHA ZAKE

Kuhusu fedha anazotumia kutumia kwa ajili ya Yanga, Zahera anasema: “Kuna nyingi hawajarudisha, walichowahi kunirudishia ni pesa ambayo niliitumia wakati tunakwenda Botswana nako viongozi walitangulia, timu ilipofika tukapokelewa na basi la wapinzani wetu (Township Rollers) tena limebandikwa mpaka picha za wachezaji wao, viongozi wanatuambia tutumie basi hilo, mimi nilishangaa na hata wachezaji walishangaa sana, nikawauliza tutumie basi la wapinzani wetu? Hii sijawahi kuona nikakataa wakasema hawana pesa nikatoa pesa zangu dola 2,000 (Sh4.5 milioni) kukodi basi, hizo niliporudi Tanzania walinirudishia, shida hapa sio kurudishiwa ni utawala bora na uwajibikaji.

“Huwezi kwenda nje kucheza mechi siku moja kabla ya kuamkia siku ya mchezo mkala chakula katika hoteli mliyofikia hilo haliwezekani, lakini Yanga hapa yanafanyika hayo, angalia siku tunakwenda kucheza na Zesco uongozi unataka tupate chakula katika hoteli tuliyofikia nikasema hapana, tukatoka nje kutafuta chakula na wachezaji kisha tukarejea hotelini, mpira wa Afrika hauwezi kufanikiwa kwa mambo ya namna hiyo.”

DENI LA SH500,000

Zahera anadai kuwa timu ya Yanga ilizuiwa hotelini jijini Mwanza, kisa ikiwa ni deni la Sh545,000 wakati wa mchezo wao dhidi ya Pyramids ambapo kabla ya hapo walivaana na Mbao FC kwa mechi ya Ligi Kuu Bara.

“Hoteli ambayo tulikuwa tumefikia ilikuwa mbovu sana, ni kama ipo Kariakoo pale katikati, hapohapo ndio tulitakiwa kukaa tucheze na Pyramids. Mimi nikasema hapana, nikaomba namba ya yule bosi wa GSM, namshukuru sana alikuwa Dubai nikamuelezea akasema kocha ngoja tutawatoa hapo, kweli kesho yake tukahamishwa na kwenda kwenye hoteli nzuri, siku tunatoka sasa nimeshapanda kwenye basi na wachezaji tunaona basi haliondoki.

“Meneja ananifuata, kocha hapa tumezuiwa timu inadaiwa Sh545,000 za gharama za vinywaji na maji, nikamwambia si ukawaambie viongozi wale pale chini, pale chini kulikuwa na (anamtaja kiongozi) na mwingine, (kiongozi huyo) akanifuata akasema kocha naomba ulipe tutakulipa tukifika.”

MKWANJA ALIOUTUMIA

“Nimesikia kuna watu wanasema nawadai Yanga Sh bilioni moja, nikacheka nawezaje kuwapa Yanga pesa zote hizo lakini kilichokuwa kinatokea ni kwamba kuna pesa nilikuwa nasaidia wachezaji kwa matatizo mbalimbali, pia hata kununua tiketi za ndege na hata kurudisha morali na haya mambo ya viongozi, naweza kusema mpaka sasa nimetumia kiasi cha dola 50,000 (takriban Sh114 milioni), sikuwa nataka kuona timu ipate aibu kubwa na fedha hizo zipo ambazo hata viongozi

walikuwa wananiomba wanajijua.”

MALENGO YA TIMU

“Tuanze na msimu uliopita, unajua msimu ule kama isingekuwa kutudhulumu na mambo ya hovyo ambayo Yanga ilifanyiwa tungechukua ubingwa, achilia mbali changamoto za maisha yetu wakati huo na hata kikosi chetu. Msimu huu tukasema tukiongezee nguvu kikosi chetu kuna watu wanaona kama timu hii haina nguvu, mimi nasema hapana kikosi chetu hiki ni bora zaidi shida tulichelewa kuunganika.

“Kwa malengo kama klabu nashangaa wananitoa sasa, lakini ukiangalia hatukuwa na malengo ya kusema tufike hatua yoyote katika Ligi ya Mabingwa au Kombe la Shirkisho na labda malengo makubwa yalikuwa ni ligi na Kombe la FA na yote hayo tuko sawa mpaka sasa, ndiyo maana nasubiri hiyo barua yao nijue wananiondoa kwa sababu ipi? Naona kama walipata tamaa baada ya kuona Yanga imeingizwa katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Mwenyekiti mwenyewe aliniambia wakati anamjibu yule mtu aliyempigia simu akimwambia anifukuze, yeye mwenyewe alimjibu kuwa hatuwezi kumfukuza kocha kwa kuwa hatukumpa malengo ya kuchukua au kufika kokote katika Ligi ya Mabingwa au hata Kombe la Shirikisho.”

KIKOSI CHA UBINGWA

“Kama watu wanakata tamaa mimi kama kocha sikati tamaa, mimi nitaondoka lakini kama kocha atakayekuja atatuliza akili vizuri na kuendelea pale tulipoishia Yanga itakuwa bingwa, ninachoomba yasitokee mambo ya kama ya msimu uliopita.

UONGOZI UNAKWAMIA HAPA

Zahera anasema, “kuna maeneo (viongozi) wanakwama hasa katika muundo wa uongozi na utaratibu mzuri vile mpira unataka, mapungufu yao ni kama hayo ambayo nimekuelezea lakini pia kuna maeneo wanajitolea vizuri kutafuta pesa kujaribu kulea timu, tangu wameingia madarakani naona wanalipa mishahara vizuri posho hayo siwezi kusema uongo.”

SHIDA NINI?

“Mimi sidhani kama ni sahihi, hilo unajua ukiangalia mechi ambazo niko hapa na zile ambazo sikuwepo nafikiri tumefanya vibaya zaidi zile ambazo mimi nilikuwa hapa.

“Angalia kuna wengine wanasema kocha Noel (Mwandila) alikuwa hawezi kazi naona kama hawajui kitu, mimi nikiondoka Noel anakuwa na majukumu yote ambayo namuachia na hata nikija naangalia mambo yako sawa? Naona yako sawa sasa hapo utasema nini.”

UONGOZI JANGWANI

Akizungumzia kwa kina kuhusu uongozi wa klabu hiyo, anasema: “Ukiniuliza tofauti ni moja au mbili, unajua wale viongozi wa mwaka jana hawakuwa na nguvu sana kutokana na hali waliyokuwa nayo, lakini kazi ilifanyika vizuri sana sababu walijua nafasi yao na ya makocha tofauti na uongozi wa sasa wao wanaingia wakiwa wapya, lakini wanatafuta nafasi ya kuingia sana kwenye mambo ya mpira ambayo sio ya kwao.

“Najua kwamba mwenyekiti alikuwa kocha, lakini anapaswa kutambua kwamba mpira hauwezi kuwa wa aina moja tu ile ya kwako kwa watu wote, makocha wanatofautiana, tulipokuwa tunakaribia kucheza na Pyramids (anamtaja kiongozi) anakuja anaanza kuelekeza Feisal unatakiwa ucheze hivi, unashuka halafu Makame unapanda, hii haiwezekani sasa wachezaji wanajiuliza sasa kocha wewe unataka tusipande mbele mbona sasa (anamtaja kiongozi) anasema tupande? Hapo shida inakuja ni tofauti na wale wa mwaka jana.

“Kwangu ilikuwa rahisi kufanya kazi na wale sababu hawakuwa wananiingilia katika majukumu na hili (anamtaja kiongozi) alifanya mara ya pili nakumbuka wakati anachaguliwa tu alikuja Iringa wakati tunacheza na Lipuli, alikuja tukiwa mapumziko, alikuja na kuanza kuelekeza kuhusu mpira, hii lazima itavuruga mambo mengi.”

TUHUMA DHIDI YA WAKONGO

“Nafikiri maneno haya mengi yametoka kwa wachezaji wapo ambao wanatoa maneno ya ajabu kutokana na wao kushindwa kuonyesha uwezo ukiangalia hakuna shabiki anakuja mazoezini na hata viongozi hawaji mara kwa mara hawajui wachezaji wako katika ubora gani.