Zahera apewa Ukurugenzi Gwambina FC

Muktasari:

Zahera amejiunga na Gwambina ambapo majukumu yake ni kusimamia idara ya Ufundi katika timu hiyo inayojiandaa kushiriki Ligi Kuu kwa mara ya kwanza.

UONGOZI wa Gwambina FC umempa shusha kikosini aliyewahi kuwa Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera ambaye atakuwa Mkurugenzi wa benchi la ufundi kwa mkataba wa miaka miwili.

Gwambina ya wilayani Misungwi jijini hapa, inajiandaa kushiriki Ligi Kuu kwa mara ya kwanza ambapo inaendelea kusuka kikosi chake ili kuanza msimu kwa kishindo.

Katibu Mkuu wa Klabu hiyo, Daniel Kirai ameithibitishia Mwanaspoti Online leo Jumanne Agosti 11, 2020 kuwa, uongozi umemleta Zahera kikosini ili kusimama idara ya ufundi akisaidiana na Makocha walioipandisha timu Ligi Kuu.

Amesema taarifa za kwamba Mkongo huyo amekuja kuwa Kocha Mkuu si za kweli isipokuwa wataendelea kubaki na Novatus Fulgence (Kocha Mkuu) akisaidiana na Athuman Bilali ‘Billo’.

“Naomba nifafanue hili ili lieleweke, ni kweli tumemleta Zahera lakini si kwamba anakuja kuwa Kocha Mkuu,  huyu ni Mkurugenzi wa Ufundi na Kocha Mkuu ni Fulgence na Msaidizi ni Billo” amesema Kirai.

Kiongozi huyo ameeleza kuwa uongozi unaendelea kurekebisha mapungufu yaliyopo kwenye Uwanja wao ili kuhakikisha ligi inapoanza Septemba 6 unakuwa sawa kwa ajili ya mechi zote zikiwamo za Simba na Yanga.

“Hizo taarifa za kwamba Uwanja wa Gwambina hauwezi kuchezewa mechi za Simba na Yanga zipuuzwe, kwa sasa tunaendelea na marekebisho na nikuhakikishie michezo yote 36 na zile za FA zitakuwa hapa Misungwi,” amesema Kirai.