Zahera: Sijaona wa kuitibulia Yanga kabisa!

Saturday December 8 2018

 

By CHARITY JAMES

KOCHA wa Yanga, Mwinyi Zahera hataki mchezo kabisa linapofika suala lá kukokotoa pointi katika mchezo wao wa Jumapili dhidi ya Biashara, na ameamua kupanga mkakati mzito kuhakikisha hawapotezi mchezo huo.
Zahera, ambaye amekuwa kipenzi cha mashabiki wa Yanga akilibeba jeshi lake katika kipindi kigumu cha ukata, ameonya kuwa anatambua ugumu wa timu za mkiani hivyo amewaweka kikao wachezaji wake na kuwapa onyo kali.
"Mechi na Biashara ni ngumu kwetu kwa sababu kucheza na timu iliyopo mkiani ni hatari kubwa, lakini nimewaambia wachezaji wangu kujiandaa kisaikolojia na kuuchukulia mchezo huo kwa muhimu mkubwa.
"Itakuwa mechi ya nguvu kwa wachezaji wangu, lakini tunataka kushinda hivyo tutapambvana hadi dakika ya mwisho uwanjani, hatutaki kupoteza mchezo kabisa," alisema.

AJIBU, NGASSA NJE
Ibrahim Ajibu ambaye alifunga bao la kusawazisha dhidi ya Prisons mchezo ambao, ulimalizika kwa Yanga kushinda 3-1 anaweza kuukosa mchezo huo kutokana na kufiwa na mama mkwe wake.
Ajibu alipatwa na tatizo hilo wakati Yanga ikiwa Sumbawanga katika mchezo wao wa kirafiki ambao, ulimalizika kwa timu hiyo kukubali kipigo cha bao 2-1 na nyota huyo kushindwa kucheza.
Zahera alisema Ajibu ameruhusiwa kwenda kushiriki msiba hivyo, hatakuwa miongoni mwa nyota wake watakaoshuka dimbani Jumapili kumenyana na Biashara.
"Sio Ajibu tu pia tunatarajia kumkosa Mrisho Ngasa, ambaye anakabiliwa na adhabu ya kadi nyekundu aliyoipata katika mchezo wetu na Tanzania Prisons," alisema Zahera.

YONDANI, TSHISHIMBI, GADIEL NDANI
Zahera alisema kikosi chake kitaongezwa nguvu kwa kurejea kwa baadhi ya wachezaji muhimu akiwemo Nahodha Kelvin Yondani.
Alisema Yondani ameanza mazoezi jana na amejiunga na wenzake kambini tayari kwa ajili ya mchezo huo, Papy Tshishimbi ambaye alikuwa nje kwa muda tayari ameanza mazoezi na ni miongoni mwa nyota watakaocheza Jumapili.
"Gadiel alipata majeraha katika mchezo dhidi ya Mwadui FC na kuruhusiwa kuondoka Shinyanga kurudi Dar es Salaam, kwa ajili ya kutibiwa sasa yupo fiti na ataungana na Yondani na Tshishimbi," alisema.

BIASHARA WATUA KAMILI
Kikosi cha Biashara kimetua jijini Dar es Salaam bila kocha na kuweka wazi kuwa, kimekuja tayari kwa kuvunja rekodi ya Yanga ya kutofungwa.
Biashara imetua jijini na jana jioni imefanya mazoezi Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam tayari kwa kuikabili Yanga.
Meneja wa Biashara United, Aman Joshua alisema kikosi kimetua bila kocha na kuweka wazi kuwa, hawana shaka kuelekea mchezo huo kwa kuwa wamejiandaa.
"Kocha anaumwa toka mechi na Lipuli hayupo benchi na tulipata matokeo mabaya katika mchezo huo kwa kufungwa bao 2-0, ila kwa Yanga tumekuja kuvunja rekodi na kubadili matokeo,” alisema.

Advertisement