Zahera: Nipo tayari kuifundisha Simba

Muktasari:

Akizungumza na Mwanaspoti, Zahera alisema yupo kimaslai zaidi kama Simba wakahitaji huduma yake yupo tayari kuwafundisha kwani ndio kazi aliyoisomea anaifanya popote bila kubagua anapopata timu yoyote lazima afanye kazi.

SIKU chache baada ya kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera kutangaza kuwa yupo tayari kuifundisha Yanga hata bila ya kulipwa amesema yupo tayari kuifundisha klabu ya Simba endapo atafukuzwa na Yanga.
Akizungumza na Mwanaspoti, Zahera alisema yupo kimaslai zaidi kama Simba wakahitaji huduma yake yupo tayari kuwafundisha kwani ndio kazi aliyoisomea anaifanya popote bila kubagua anapopata timu yoyote lazima afanye kazi.
''Hakuna kazi ya ajabu kama ya mpira unaweza ukawa mwalimu wa timu ya Yanga na tunakinzana na kocha wa Simba pamoja na mashabiki lakini ikitokea nikahamia Simba nakuhakikishia kabisa nitapendwa na mashabiki kila nitakapopata matokeo mazuri," alisema.
"Pia mpira ni kitu cha ajabu, kwasasa Yanga tunashinda na mashabiki wananipenda wanasema kocha mzuri lakini tukifungwa mechi 5 mfululizo watanikataa na kunifukuza, sasa Simba wakija nitakaa vipi wakati mimi ni kocha'', alisema Zahera.
Aidha kocha huyo raia wa Congo aliongeza kuwa anafanya kazi Yanga kwa mapenzi yake yote lakini ukifika muda timu haipati matokeo ni ngumu viongozi kumvumilia lazima watamuondoa.
Zahera ameiwezesha Yanga kuongoza ligi kuu soka Tanzania bara ikiwa na alama 50 kwenye mechi 18 ilizocheza ikiwa imeshinda michezo 16 na kutoa sare miwili.