Zahera: Tunatinga makundi Afrika na kubeba ubingwa Ligi Kuu Bara

Muktasari:

Zahera aliliambia Mwanaspoti kuwa hata timu za Ulaya hufungwa, lakini mwisho hutangaza ubingwa,hivyo hawawezi kukata tamaa kwa matokeo ya mchezo wa kwanza.

KOCHA mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera ametamba kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kutokana na mikakati waliyojiwekea msimu huu na kwamba kila kitu kinawezekana kufikia malengo.
Yanga ilianza kwa kupoteza mchezo wake wa Ligi Kuu Bara ikifungwa na bao 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting matokeo ambayo yalionekana kuwaumiza sana wanachama na mashabiki wa timu hiyo.
Kutokana na hilo, Zahera amewaambia mashabiki wake kuwa licha ya kuanza vibaya msimu huo lakini mipango yao ya kutwaa ubingwa ipo pale pale.
Zahera aliliambia Mwanaspoti kuwa hata timu za Ulaya hufungwa, lakini mwisho hutangaza ubingwa,hivyo hawawezi kukata tamaa kwa matokeo ya mchezo wa kwanza.
Kocha huyo mwenye ushawishi mkubwa Jangwani, alisema malengo ya timu kwa sasa ni kuhakikisha wanafuzu kwanza hatua ya makundi ya ligi hiyo ya mabingwa  huku hesabu zingine ikiwa ni kubeba taji la Ligi Kuu Bara.
“Mechi moja tu ndio itupotezee ndoto za Ubingwa?, Barcelona waliwahi kufungwa mechi ya awali kabisa lakini walitangaza ubingwa, kwahiyo hata sisi Yanga itakuwa hivyo”alitamba Zahera.
Kocha huyo hakusita kuwasifia nyota wake akisema wanampa furaha kutokana na jinsi wanavyomuelewa mazoezini na kwamba mchezo wao na Zesco utakaopigwa Septemba 14 uwanja wa Taifa lazima wafanye kweli.
“Nashukuru vijana wanaenda vizuri wananielewa ninachowaelekeza, hata ambao hawapo kambini lakini huko walipo kwenye timu ya Taifa wanafanya mazoezi kwahiyo sioni tatizo” alisema Zahera.