Zabibu: Banda ni sukari ya warembo

Muktasari:

Zabibu Kiba anasema mume wake anayeitwa Abdi Banda ana mapenzi makubwa na timu yake na huwa hapendi masihara katika kazi yake hiyo kwani, akipata matokeo mazuri anakuwa na furaha ya kupitiliza hadi nyumbani, lakini ikitokea wamefungwa anakosa amani na huwa anabadilika.

JANA Ijumaa tulianza makala ya mke wa beki wa klabu ya Baroka FC ya Afrika Kusini, Abdi Banda, Zabibu Kiba ambaye alifunguka mambo mengi kuhusiana na maisha yake ya ndoa.
Pia, alieleza vitu vingine ikiwemo ushabiki wa timu za Ulaya na muziki wa Bongo Flava, ambao umetekwa na kambi za mastaa Ali Kiba na Diamond Platnumz.
Hapa Zabibu, ambaye ni mdogo wa King Kiba anafichua jinsi mumewe anavyozimia na muziki na msanii ambaye anapenda kusikiliza kazi zake zaidi anapokuwa ametulia.

DIAMOND, BANDA HAYUMO
“Kiukweli Banda anapenda sana muziki hasa Bongo Flava na mara nyingi anasikiliza nyimbo bila kubagua. Yaani yeye anapenda kazi nzuri na hana kambi kati ya Kiba wala Diamond, huwa anasikiliza nyimbo inayomvutia.
"Mume wangu muda mwingi akiwa nyumbani anapenda kusikiliza muziki, lakini hana msanii maalumu na ndio sababu nimeshindwa kumjua katika kipengele hicho.
"Nyimbo za Kiba huwa anasikiliza kabla hata hazijatoka, ila kifupi ni mtu anayependa muziki kwa ujumla, swali kubwa analouliza kuhusu mziki ni nyimbo gani mpya imetoka," anasema.

KUCHORA TATUU
Ni kawaida kwa wake wa mastaa wa soka duniani, kuchora tattoo sehemu za miili yao kama ilivyo kwa mke wa Amissi Tambwe wa Yanga, ambaye ameandika jina la mumewe katika mkono wake, lakini kwa Zabibu ni tofauti kabisa na mambo hayo.
"Kwanza dini hairuhusu pia mume wangu hapendi hayo mambo ya kuandikana kwenye mwili, upendo upo moyoni tunapendana kila mmoja anafahamu hilo inatosha, hiyo michezo ya kuchora mwilini haimanishi ndio upendo wa kweli," anasema.

UWANJANI MARA MOJA TU
Anaweka wazi kuwa yeye alikuwa shabiki wa Simba hapo zamani kabla hata ya kuingia katika mahusiano na Banda, lakini sasa ni shabiki mkubwa wa Baroka kutokana na timu hiyo kuwapa ulaji na ndio sehemu ambayo mume wake anaifanyia kazi.
"Tangu nimeanza mahusiano na Banda ni mara moja tu nimeenda uwanjani na kumuona akicheza, lakini muda wote akiwa na mpira na akifuatwa na wapinzani wake waliokuwa wanacheza naye nilikuwa nachanganyikiwa kwa sababu nahofia wanaweza kumchezea vibaya."
"Napenda kazi ya mume wangu, napenda muda wote acheze bila kupata matatizo kiukweli siku hiyo niliyokwenda uwanjani nilikosa raha hadi mwisho wa mchezo na naamini kila aliyekuwa karibu yangu alitambua hilo. Nilikuwa napiga kelele za maumivu na sio furaha," anasema.

AKIFUNGWA ANAPAGAWA
Mume wangu ana mapenzi makubwa na timu yake na huwa hapendi masihara katika kazi yake hiyo kwani, akipata matokeo mazuri anakuwa na furaha ya kupitiliza hadi nyumbani, lakini ikitokea wamefungwa anakosa amani na huwa anabadilika.
"Nimeshamsoma katika hali zote timu yake ikishinda na ikifungwa hivyo, hainipi tabu najua namna ya kukaa naye japo kuwa ya matokeo mabaya ni sehemu ya changamoto, lakini inamnyima raha muda wote."
"Nafurahia maisha yetu kwani kila mmoja anafahamu mapungufu ya mwenzake hivyo, tunaishi kwa amani na furaha ndani ya ndoa suala ambalo linaweza kutufanya tukaishi muda mrefu bila kugombana," anasema Zabibu.

MADEMU WANAMSUMBUA
"Nafahamu Mume wangu ni maarufu hawezi kukosa kusumbuliwa na wanawake, hilo suala lipo na mara nyingi nimekuwa nikionyeshwa meseji za wanawake wanaotamani kuwa na mahusiano na Banda yote ni kujenga uaminifu katika ndoa yetu."
"Nafahamu hayo yote kupitia kwa kaka zangu AbduKiba na Alikiba kutokana na umaarufu wao, wamekuwa wakisumbuliwa sana hivyo, baada ya kuolewa na Banda nilitegemea kukutana na changamoto hiyo."

ANACHOFIKIRI SASA
Mimi ni mpenzi wa Manchester United na nilikuwa navutiwa na Christiano Ronaldo kutokana na upambanaji wake uwanjani na kuwa ni mchezaji, ambaye anacheza kwa malengo natamani mume wangu afikie anga hizo."
"Wanacheza nafasi tofauti na mume wangu, lakini natamani siku moja Banda afikie mafanikio hayo na kuwa maarufu duniani."

Je unafahamu maisha ya Zabibu na mama mkwe wake kule mjini Tanga, kesho Jumapili mama mzazi wa Banda, Mwanahawa Mwalimu atafunguka kila kitu hapa hapa ndani ya Mwanaspoti.