Yondani, Abdul waliamsha Yanga

UONGOZI wa Yanga jana na leo Agosti 5, 2020 umekutana na wachezaji wake wawili, wakongwe, Kelvin Yondani na Juma Abdul kuhusu usajili wao lakini hata hivyo wameshindwa kufikia muafaka.

Yondani alikutana na viongozi jana Jumanne wakati Abdul alitinga makao makuu ya leo Jumatano lakini hata hivyo wachezaji wote wawili walishindwa kukubali ofa iliyowekwa na viongozi wao kwa ajili ya kumwaga wino kwenye mikataba mipya.

Wiki hii Yanga ilitangaza kuachana na wachezaji 14 na kuwabakisha 17 tu huku ikikiri kuwa Abdul na Yondani wamemaliza mikataba na watafanya mazungumzo nao kwa ajili ya kuongeza mikataba mipya kwani ni wachezaji wakongwe waliodumu na timu hiyo kwa muda mrefu na wanawahitaji.

Habari zinadai kuwa uongozi umewawekea ofa ndogo na ndio maana wachezaji hao wameshindwa kukubaliana nayo na sasa wanakwenda kutafakari kabla ya kuja na uamuzi wao.

Uongozi wa Yanga kupitia kwa Ofisa Habari wao, Hassan Bumbuli alisema ni kweli wamekutana na wachezaji hao kwa nyakati tofauti na kuwapa mapendekezo yao na wanasubiri mrejesho wao.

"Tulimpa Juma mapendekezo yetu na yeye akatoa ya kwake, kwa Yondani tulimpa ya kwetu lakini yeye hakutoa akasema atakwenda kujadiliana na familia yake,"alisema Bumbuli.

Yanga imetangaza kuwaacha Mrisho Ngassa,David Molinga,Andrew Vincent,Papy Kabamba Tshishimbi, Jafary Mohammed, Tariq Seif na Mohammed Issa Banka ambao mikataba yao imemalizika . Pia inaendelea na kuzungumza na wachezaji Ali Sonso,Muharami Issa, Ali Ali, Yikpe Gislain, Patrick Sibomana na Mohammed Issa 'Banka' ili kuvunja mikataba yao. Hatahivyo Sibomana tayari ametangaza kuachana na Yanga na amewatakia kila la kheri.

Timu hiyo imewabakisha kikosini wachezaji 14 ambao ni Faroukh Shikalo, Ramadhan Kabwili, Metacha Mnata,Feisal Salum,Juma Mahadhi,Adeyum Saleh, Said Makapu, Balama Mapinduzi,Deus Kaseke,Ditram Nchimbi,Abdulaziz Makame na Paul Godfrey.