Yanga yazigomea adhabu za Bodi ya Ligi, yashtaki CAF

Muktasari:

Tulipeleka malalamiko yetu mengi kwa wasimamizi wa ligi ili hatukupewa majibu, kwa maana hiyo tumeandika barua kwa Shirikisho la soka Tanzania (TFF), CAF, FIFA, Takukuru na mamlaka nyingine husika kulalamika juu suala hilo

Dar es Salaam.Uongozi wa Yanga umesema hawakubaliani na adhabu walizopewa na Bodi ya Ligi kwa wachezaji wao pamoja na klabu hiyo kwa ujumla tayari wameandika barua kwa Shirikisho la soka Tanzania (TFF), CAF, FIFA, Takukuru na mamlaka nyingine kulalamika juu ya suala hilo.

Kamati ya Saa 72, Shirikisho la Soka Tanzania hivi karibuni ilitoa adhabu mbalimbali pamoja na faini kwa klabu ya Yanga pamoja na wachezaji kutokana na makosa mbalimbali.

Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi (TPLB), Steven Mguto alitangaza kuwafungia mechi tatu na faini ya Sh 500,000 kwa wachezaji wa Yanga, Ramadhani Kabwili, Mrisho Ngassa, Cleofas Sospeter baada ya kugoma kutoka uwanjani katika pambano la ligi dhidi ya Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya.

Pia, Yanga ilipigwa faini nyingine ya Sh 500,000 baada ya kushindwa kuwakilisha kikosi chake katika mechi ya ligi dhidi ya Tanzania Prison, lakini katika mchezo dhidi ya Simba Yanga walipigwa faini nyingine ya Sh 200,000 kwa wachezaji na benchi la ufundi kushindwa kutumia vyumba rasmi vya kubadilishia nguo na faini nyingine ilikuwa ya Sh 500,000 baada ya mashabiki wake kuwarushia chupa waamuzi.

Akizungumza na makao makuu ya Yanga, Afisa habari wa klabu hiyo, Hassan Bumbuli alisema Kamati ya saa 72 imeamua kuwafungia wachezaji wao pamoja na kuipiga faini timu kwa makosa waliotaja mbalimbali.

"Yanga hatukubaliani na adhabu hizo kwani kuna mambo mengi ya kisheria hayakufuatwa mpaka kuamua kutoa hukumu hiyo.

“Tulipeleka malalamiko yetu mengi kwa wasimamizi wa ligi ili hatukupewa majibu, kwa maana hiyo tumeandika barua kwa Shirikisho la soka Tanzania (TFF), CAF, FIFA, Takukuru na mamlaka nyingine husika kulalamika juu ya hilo," alisema Bumbuli.

Katika hatua nyingine Bumbuli aligusia suala la mkutano mkuu wa Februari 16, akitaja vitu vya msingi wanavyotaka kuvirekebisha katika katiba ya sasa.

"Katiba yetu hakuna mahala inataja uongozi kupokea au kutoa fedha kupitia mitandao ya simu, lakini kwa dunia ya sasa ni ngumu kuepeka hilo kwahiyo tutakwenda kuangalia hili.

“Jambo lingine tutafanya katika mkutano ni kusajili wanachama kimfumo mpya wa kisasa kwa maana ya kieletroniki ili kufahamu idadi kamili ya wanachama wetu," alisema Bumbuli.