Yanga yawavizia Simba kijanja

VIONGOZI wa YANGA wamesema ziara yao Kanda ya Ziwa katika mechi zao tatu sio tu kutafuta ushindi, lakini wanatengeneza hesabu za kukabiliana na Simba.

Kwa mujibu wa ratiba ya Ligi Kuu Bara, Yanga inakutana na Simba Novemba 7 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ukiwa ni mchezo wa kwanza kati ya timu hizo kongwe zaidi nchini.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Mhandisi Hersi Said amesema kuwa uwepo wa timu yao katika mechi tatu za Kanda ya ziwa wakiwa wameshamalizana na KMC wakiwafuata Biashara United, kisha kumaliza na Gwambina hatua ya kwanza ni kutafuta ushindi katika mechi zote hizo.

“Tuna malengo ya msimu huu ambayo yanakamilika kwa kila mchezo kuhakikisha tunashinda, nafikiri kocha wetu alishafafanua kila kitu wakati anatua hapa, tunataka kuwa tunashinda kila mchezo ulio mbele yetu.

“Hii ndio sababu hata viongozi tumebaki huku tukihakikisha kocha wetu anapata kila hitaji lake ili kwa pamoja tuweze kufikia malengo yetu,” alisema na kuongeza kuwa hatua ya pili ni kuhakikisha kazi ya kutengeneza muunganiko inakamilika haraka ambapo

wanatambua baada ya mechi hizo watakutana na watani wao, Simba.

“Baada ya mechi hizi tatu tuna mchezo mwingine mgumu zaidi dhidi ya Simba, kwa hiyo mechi hizi pia ni sehemu ya maandalizi yake.

“Tulichoona katika mechi hizi saba tumeshinda sita na kutoa sare moja, picha tunayoipata tuna timu imara sana, muhimu sasa ni makocha kumalizia kazi yao ya kutengeneza muunganiko kwa kuwa wachezaji hawa na makocha ni wapya.

“Tutakwenda kukutana na Simba ambayo hatutaki kukutana nao tukiangalia yanayoendelea ndani ya klabu yao wala kuangalia matokeo yao yaliyopita, tutajiandaa kama tunakutana na Simba ambayo imekaa pamoja muda mrefu na wana makocha wanaoijua timu yao,” aliongeza Hersi ambaye timu yake inacheza na Biashara leo.