Yanga yaitisha Simba

Muktasari:

Huu ni mchezo wa nne kuikutanisha Yanga na Lipuli FC tangu  ilipopanda Ligi Kuu Bara msimu uliopita.  Yanga wameonekana watemi zaidi kwa kuibuka na ushindi mara mbili huku mara moja wakitoka sare.

YANGA inafahamu kuwa itakuwa nyuma kwa pointi tano ikiwa Simba itapata ushindi kwenye mechi zote za viporo za Ligi Kuu Bara,  sasa imeamua kutumia mbinu za kimafia ili kuendelea kuwapa presha wapinzani wao hao.
Miongoni mwa mbinu hizo ni kuhakikisha kuwa, inapata ushindi mfululizo kwenye mechi zake za Ligi Kuu Bara kisha kuwatazama Simba, wakipambana na hali yao wakati wenyewe wakikamilisha hesabu zao.
Baada ya kufanya hivyo kwa kupata ushindi dhidi ya Alliance, Mbao na KMC, hesabu na mpango wao huo leo Jumamosi unahamia pale kwa Kamwene mjini Iringa ambako, watapepetana na Lipuli FC kwenye Uwanja wa Samora.
Ushindi kwenye mechi hiyo utafanya pengo la pointi 70 ambazo zitakuwa 19 zaidi ya zile 51 ambazo Simba wamekusanya huku pia wakiwa mbele ya Azam wanaoshika nafasi ya pili kwa tofauti ya pointi 16.
Ni mchezo wa nne kuzikutanisha timu hizo tangu Lipuli ilipopanda Ligi Kuu msimu uliopita, ambapo Yanga wameonekana watemi zaidi kwa kuibuka na ushindi mara mbili huku mara moja wakitoka sare.
Kukosekana kwa kiungo mshambuliaji Ibrahim Ajibu na mabeki wawili wa kati, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Juma Abdul na Andrew Vincent ‘Dante’ kwa sababu tofauti kunaweza kuiweka pagumu Yanga kwenye mchezo huo.
Ajibu ndiye amekuwa mpishi wa mabao ya Yanga msimu huu, ambapo hadi sasa amepiga pasi 15 zilizozaa mabao lakini Ninja na Dante ndio mhimili wa safu ya ulinzi ambayo kuelekea mchezo huo imebakia na mchezaji mmoja tu tegemeo, ambaye ni Kelvin Yondani.
Lakini, kama ilivyo kwa Seleman Matola, Yanga pia itamkosa kocha wake mkuu Mwinyi Zahera, ambaye hajaambatana na kikosi chake mkoani Iringa, akibaki jijini kujiandaa na safari ya kurejea nchini kwao DR Congo kwa majukumu ya timu ya Taifa.
Hata hivyo, hilo linaonekana kama sio pengo kubwa kwa Yanga kwani jukumu la kusimamia benchi la ufundi limebaki kwa msaidizi Noel Mwandila, ambaye ni miongoni mwa makocha wanaoifahamu vyema Ligi Kuu na katika kulithibitisha hilo, hata Zahera mwenyewe ameonyesha matumaini kwa msaidizi wake.
“Tumefanya maandalizi kabla ya kuelekea Iringa lakini mimi ninaondoka kwenda Congo na Noel ambaye atasimamia timu dhidi ya Lipuli.
“Sina shaka naye na naamini ataiongoza vyema timu kupata ushindi ingawa tunajua kuwa Lipuli ni timu nzuri,” alisema Zahera.
Kwa upande wa Mwandile aliyekabidhiwa timu na Zahera kwa sasa alisema; “Wachezaji hao kweli hawapo, kuna wanaoumwa na wengine wana adhabu. Wapo wengine wataifanya kazi vizuri hivyo, hakuna presha katika mchezo huo.
Pigo kubwa kwa wenyeji ni kukosekana kwa Matola, ambaye atakuwa nje akimalizia adhabu ya kufungiwa mechi mbili kwa kosa la kupinga uamuzi wa refa kwenye mchezo ambao Lipuli walipoteza ugenini dhidi ya Kagera Sugar, Machi 3.
“Tunawaheshimu Yanga kama timu kubwa na inayoongoza ligi lakini inawezakana kupata matokeo mazuri dhidi yao ikiwa wachezaji watafanyia kazi kile walichoelekezwa na kutofanya makosa yanayoweza kuwapa nafasi wapinzani wetu kutuadhibu,” alisema Matola.