Yanga yaigomea hukumu ya Morrison

Wednesday August 12 2020

 

By Mwandishi Wetu

MUDA mfupi baada ya winga Bernard Morrison kutangazwa kushinda shauri na kuwa mchezaji huru dhidi ya waajili wake wa zamani Yanga, uongozi wao umesema watakata rufaa.

Mwenyekiti wa kamati ya Hadhi, Sheria za Wachezaji, Elias Mwanjala alitangaza hukumu hiyo baada ya sakata hilo kuchukua siku tatu likisikilizwa.

Uongozi wa Yanga kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii umetoa taarifa kuwa haujaridhishwa na uamuzi huo na watakata rufaa katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Michezo (CAS).

Yanga wamesema wanasubiri nakala ya hukumu kutoka kamati husika ili waanze kuchukua hatua.

“Uongozi unawataka wanachama na wapenzi wawe watulivu na kuendelea kushirikiana na uongozi katika maeneo mbalimbali ya klabu” imesomeka taarifa hiyo

Wameongeza “Aidha uongozi utaendelea kushirikiana na wadhamini wetu katika kujenga klabu yetu”

Advertisement

Katika maamuzi yaliyotolewa na TFF ni kuwa mchezaji huyo yupo huru na atachagua timu ya kucheza baada ya mkataba baina ya Yanga na Morrison kuwa na mapungufu

"Kikao kilikuwa kirefu mpaka kufikia maamuzi haya, malalamiko ya Morrison yalikuwa kwamba hakuongeza mkataba na Yanga, tumeangalia mkataba wake tumeona una walakini tumeona Yanga mkataba wao una utata kidogo," amesema Mwanjala

Hata hivyo, Morrison atapelekwa kamati ya maadili baada ya kusaini mkataba na klabu ya Simba Agosti 8, 2020.

Advertisement