Yanga yaichimba mkwara Simba

Muktasari:

Yanga imepoteza michezo mitatu ya mwisho waliyokutana na Simba, kwa msimu huu wamepoteza kwa kipigo cha mabao 3-1 katika mzunguko wa kwanza, mchezo ambao ulipigwa dimba la Karume, Dar es salaam.

Dar es Salaam. TIMU ya Yanga Queens imepiga mkwara mzito kwa wapinzani wao, Simba Queens, wanaoatarajia kucheza mechi ya Ligi Kuu ya Wanawake keshokutwa Ijumaa kwenye Uwanja wa Mo Simba Arena uliopo Bunju jijini Dar es Salaam.

Kocha Mkuu wa Yanga, Edna Lema alisema itakuwa mechi ngumu kwa pande zote mbili, lakini wao hawatakubali unyonge mbele ya Simba. “Sitaki kusema kuwa itakuwa ni mechi rahisi kwa kuwa Simba imekuwa na kiwango bora msimu huu, pia ni mechi ambayo huwezi kuiamua kwa matokeo ya mechi zilizopita kwa sababu ni mechi ambayo kila timu itakuja tofauti kwa kuwa ni mechi nzuri,” alisema

Yanga imepoteza michezo mitatu ya mwisho waliyokutana na Simba, kwa msimu huu wamepoteza kwa kipigo cha mabao 3-1 katika mzunguko wa kwanza, mchezo ambao ulipigwa dimba la Karume, Dar es salaam.

Licha ya kuwa na rekodi mbaya mbele ya wapinzani wao, Edna alisema hilo halimtishi. “Tunatakiwa kwenda kujiuliza kwa kuwa wametufunga mara tatu mfululizo, hivyo tunaenda kukaa chini ili kuangalia wapi tunakosea,” alisema.

Yanga ambayo imetoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Mlandizi Queens katika mchezo wao wa mwisho wa ligi ambao ni wa kwanza tangu kusimamishwa kwa sababu ya janga la virusi vya corona, wanashika nafasi ya tano baada ya kukusanya alama 23 katika michezo 14.

Baada ya mechi hiyo kumalizika Lema pia alieleza sababu za kutoka sare.

“Unajua ni mechi ya kwanza tokea michezo iruhusiwe, lakini wachezaji walionyesha kiwango bora japokuwa kulikuwa na makosa madogomadogo ambayo tulifanya nayo yalichangia kutugharimu, pia kuna matukio ambayo hayakuwa sawa kimchezo waliyofanya timu pinzani japokuwa mwamuzi labda hakuyaona, lakini yote kwa yote tunamshukuru Mungu.” Katika mchezo huo mabao ya Yanga yalifungwa na Grace Mbelay na Fatuka Bushir, huku mabao ya Mlandizi yakifungwa na Zainabu Dudu na Emiliana Mdimu.