Yanga ya Zahera na maajabu yake

Muktasari:

Kocha wake, Mkongomani Mwinyi Zahera hataki mchezo na Yanga yake amekuwa msisitizaji wa nidhamu ambayo anaamini inaweza kuibeba timu hiyo kutwaa ubingwa huo misimu huu wa 2018/19. Mpaka sasa, Yanga inaongoza Ligi Kuu (TPL), ikiwa na pointi 50, wapinzani wake Azam FC na Simba wakifuata nyuma.

MIONGONI mwa timu 20 zinazoonekana kuwa siriazi kuuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) ni Yanga ambayo pamoja na kuwa na hali mbaya kiuchumi lakini imeweza kujikusanyia idadi kubwa ya pointi.

Kocha wake, Mkongomani Mwinyi Zahera hataki mchezo na Yanga yake amekuwa msisitizaji wa nidhamu ambayo anaamini inaweza kuibeba timu hiyo kutwaa ubingwa huo misimu huu wa 2018/19. Mpaka sasa, Yanga inaongoza Ligi Kuu (TPL), ikiwa na pointi 50, wapinzani wake Azam FC na Simba wakifuata nyuma.

Azam imeachwa alama 10 na vinara wa ligi hiyo, ikiwa mchezo mmoja nyuma huku Wekundu wa Msimbazi wameachwa pointi 17, wakiwa na mechi nne mkononi.

Mwanaspoti linakuletea maajabu ambayo yametokea tangu kuanza kwa msimu huu kwenye kikosi cha Yanga SC, kikiwa chini ya Kocha Zahera ambaye amegeuka kuwa kipenzi cha mashabiki na wanachama wa timu hiyo.

MATAJIRI WA JEZI

Timu zote za Ligi Kuu Tanzania Bara zimekuwa na utaratibu wa kutambulisha jezi zao mpya mwanzoni mwa msimu ambazo zitatumika katika msimu husika kama tulivyoshuhudia timu kadhaa zikifanya hivyo. Mbeya City na Simba zilifanya hivyo lakini kwa Yanga imekuwa tofauti.

Yanga msimu huu imekuja kivingine kabisa imeshindwa kufanya hivyo na imeonekana kuwa na jezi zaidi ya tano ambazo imekuwa ikizitumia katika michezo ya ligi pamoja na ile ya Kombe la Mapinduzi. Ilipocheza na African Lyon pia ilivaa jenzi mpya, wakati wa mchezo wa FA dhidi ya Tukuyu Stars ilifanya hivyohivyo.

MWENDO WA BAKULI

Yanga ni miongoni mwa klabu kubwa Afrika lakini imekosa uwekezaji wa kuisaidia katika kulipa mishahara ya wachezaji wake na mambo mbalimbali ya kuiandaa timu ikiwa ni pamoja na usajili.

Katika kitu kisichokuwa cha kawaida msimu huu klabu hiyo imekuwa na kampeni ya kuchangishana fedha kwaajili ya kuikwamua kwenye lindi la umasikini ikiwa ni pamoja na posho kwa wachezaji na usafiri. Utaratibu huo umekuja chini ya Kocha Zahera ambaye ameweka wazi timu ni ya wanachama haoni sababu ya kuwaomba waichangie.

KIKOSI B

Katika hali ambayo haikutarajiwa na wengi ni kitendo cha Kocha Zahera kupeleka kikosi B katika Kombe la Mapinduzi na kuweka wazi sababu kubwa ya kufanya hivyo ni kutokana na kutokuwa na kikosi kipana. Zahera alisema hana kikosi kipana kama ilivyo kwa timu nyingine hawezi kupeleka kikosi chake cha kwanza na alibaki nacho Dar es Salaam akikinoa kwa mwendelezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

TUZO

Ukiwa ndio kwanza nusu msimu wa Ligi Kuu tayari Zahera ameiongoza Yanga kushinda michezo 16 kati ya 18 iliyocheza na amebeba tuzo tatu za Kocha Bora kitu ambacho sio cha kawaida na hakijawahi kutokea. Achana na tuzo zake hizo pia amewaongoza vijana wake kutwaa tuzo.

Wakati Mkongomani huyo akibeba tuzo ya tatu, mshambuliaji wake kutoka DR Congo, Heritier Makambo ameshachukua mbili mfululizo na ndiye mchezaji anayeongoza kwa upachikaji mabao hadi sasa akiwa na mabao 11 kwenye Ligi Kuu.

REKODI

Yanga ndio timu pekee ambayo haijapoteza mchezo Ligi Kuu Bara, inatesa kileleni ikiwa na pointi 50 baada ya kutoa sare mbili, suluhu ya Septemba 30 na Simba kisha dhidi ya Ndanda FC imefunga jumla ya mabao 35 na nyavu zake kuguswa mara 12.

AJIBU NAHODHA

Wengi hawakuamini kusikia Mkongo huyo amemvua unahodha, beki wake, Kelvin Yondan na kumpa Ibrahim Ajibu. Ilikua Januari 4 mwaka huu Zahera alipofanya mageuzi hayo na kuweka wazi sababu ya kufanya hivyo ni kutokana na Yondani kushindwa kufika mazoezini bila ya kutoa sababu.

Suala hilo lilizua mijadala mingi katika mitandao ya kijamii na hakueleweka na baadhi ya wapenda soka lakini msimamo wake ulibaki palepale. Kocha Zahera aliweka wazi anaendesha mpira kwa kusimamia nidhamu huku akisisitiza mchezaji aliyekosa nidhamu hana nafasi katika kikosi chake.

kitendo hicho kilimgusa meneja wa kikosi hicho, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ambaye alisema amepokea kwa masikitiko taarifa hizo kwasababu yeye ndiye alimkabidhi Yondani kitambaa cha unaodha baada ya kustaafu.

NDOA YA KAKOLANYA

Ulianza kama utani lakini sasa imekuwa kweli, hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya Kocha Zahera kubaki na msimamo wake wa kutokukubali kumrudisha, kipa namba moja wa Yanga, Beno Kakolanya katika kikosi chake kutokana utovu wa nidhamu.

Zahera alisema kama Wanayanga wanamtaka Kakolanya arudi Yanga, basi wachague mmoja kati yake na kipa huyo abaki klabuni. Suala hilo limeonekana kuwa gumu kwa viongozi wa timu hiyo na kukubaliana na uamuzi wa kocha huyo.

Tayari Kakolanya na wakili wake wamepeleka ombi la kuvunja mkataba na Yanga ili awe huru, hivyo atakuwa huru kujiunga na timu yoyote anayoitaka.