Yanga wamzingua Mwamnyeto

Muktasari:

Matajiri wa Simba na Yanga, waliingia kwenye vita ya kugombea saini yake, ingawa bado hilo halijahitimishwa kwani hajasaini rasmi kwenye timu yoyote licha ya kwamba, mambo mengi wameshaafikiana.

BEKI wa Coastal Union, Bakari Mwamnyeto ameweka wazi changamoto anayoipata kutoka kwa mashabiki wa timu hiyo, kumuona anawazuga na kusubiri kutimkia Yanga ambako alikuwa anahusishwa kusajiliwa msimu huu.

Matajiri wa Simba na Yanga, waliingia kwenye vita ya kugombea saini yake, ingawa bado hilo halijahitimishwa kwani hajasaini rasmi kwenye timu yoyote licha ya kwamba, mambo mengi wameshaafikiana.

Katika stori za hapa na pale alizopiga na Mwanaspoti jana, Mwamnyeto alifunguka kuwa baada ya dili lake la kutimkia katika timu hizo kutawaliwa na ukimya, mashabiki wa Coastal Union, hawakumfumbia macho waliamua kumpiga madongo kiana kuwa anawatosa kisa pesa.

Alisema amekuwa akiwasikia mashabiki wakimwambia licha ya kuchezea timu yao, lakini hana lolote akili yake ipo kwenye timu yake mpya ya Yanga na kwamba hata ikitokea akafanya kosa la kibinadamu anakuwa anawaza kufikiriwa vibaya.

“Kuna wakati mwingine mchezaji anaweza akafanya makosa ya kibinadamu, lakini utasikia huyo anawaza timu yake mpya Yanga, hili ni changamoto inayonifanya kuwa mwangalifu ninapoaminiwa kupewa dakika za kucheza na kocha kuzitumia kwa umakini zaidi,” alisema na kuongeza: “Wakati mwingine ukipita mtaani utasikia wewe unaenda lini Yanga ama unasubiri ligi iishe,. Wapo wanaoongea kwa kejeli na wengine kwa wema kujua kama nilimalizana nao au lah!”

Alipoulizwa je bado Simba na Yanga, zinaendelea kukufuatilia? Alijibu “Ndio bado kuna mazungumzo yanaendelea ingawa meneja wangu ndiye mwenye mamlaka na hilo. Timu itakayokuwa tayari nitaitumikia, nipo kwa ajili ya kucheza hivyo meneja akiniambia utakwenda huku ama nje ya nchi, nitakuwa tayari,” alisema.

Mwamnyeto ameshazungumza na timu zote mbili na Yanga walimpelekea mkataba wa awali lakini akagoma hadi meneja wale arudi nchini mwisho wa msimu.