Yanga wafunga mtaa Arachuga

Muktasari:

Yanga na Leopards zitavaana Jumapili kwenye uwanja huo na CCM imeamua kurekebisha maeneo ya majukwaa, sehemu ya kuchezea na hata miundombinu ya maji na vyoo kusudi mashabiki wapate burudani bila kero yoyote.

UJIO wa Yanga jijini Arusha imekuwa kama neema kwa wadau wa soka na wamiliki wa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, ambao wameamua kuufunga kwa muda uwanja huo ili kuboresha mambo kabla ya kuipisha timu hiyo kumalizana na AFC Leopards ya Kenya jijini hapa.

Yanga itakuwa Arusha kuanzia Agosti 17 ili kucheza na Leopards ikiwa sehemu ya maandalizi ya mchezo wa marudiano dhidi ya Township Rollers ya Botswana na wamiliki wa uwanja huo CCM wameufunga ili kuutengeneza ili kukidhi mahitaji ya mechi hiyo ya kimataifa.

Yanga na Leopards zitavaana Jumapili kwenye uwanja huo na CCM imeamua kurekebisha maeneo ya majukwaa, sehemu ya kuchezea na hata miundombinu ya maji na vyoo kusudi mashabiki wapate burudani bila kero yoyote.

Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Gerald Munisi alisema wametenga Sh 5-7 milioni kuboresha lengo la kuufanya uwanja huo kurudi katika hadhi yake ya awali ili kupata michezo mingine mingi ya kimataifa.