Yanga hii jifanye kama unajikuna

Muktasari:

  • Yanga sasa inaongoza Ligi kuu Bara ikiwa na pointi 41, wakifuatiwa na Azam (39) na Simba ipo nafasi ya tatu na pointi zake 27.

MASHABIKI wa Simba walikuwa na furaha baada ya Biashara United kuitangulia Yanga na kuandika rekodi ya kuwa timu ya kwanza kati ya sita zilizopanda Ligi Kuu kugusa nyavu za Vijana wa Jangwani, lakini walijikuta wakikatwa stimu baada ya Shaibu Ninja na Heritier Makambo kupindua matokeo kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar.

Mashabiki hao wa Simba waliokuwa wakiishangilia Biashara iliyotangulia kupata bao dakika ya 38 kupitia kwa beki wa kushoto, Abdulmajid Mangalo aliyepanda mbele lakini ghafla walilazimika baada ya Ninja kufunga bao la kusawazisha dakika ya 70.

Ninja alifunga bao hilo akimalizia pasi murua ya mtokea benchi, Amissi Tambwe na kuipa afueni Yanga waliokimbizwa kwa muda mrefu na wapinzani wao, huku ikishuhudia, Kelvin Yondani na Papy Kabamba Tshishimbi wakirejea tena uwanjani.

Yondani alishindwa kuitumikia Yanga tangu aliporudi na timu ya taifa, Taifa Stars iliyoenda kucheza na Lesotho, huku Tshishimbi alikuwa majeruhi kwa muda mrefu.

Katika mchezo wa jana Jumapili winga mpya wa Yanga, Ruben Bomba alifunika baada ya kupokewa kwa shangwe na mashabiki wa Yanga alipotinga uwanjani hapo na kwenda jukwaani kuishuhudia timu yake tarajiwa.

Licha ya kushinda vijana wa Mwinyi Zahera huenda hawaamini kama walicheza na Biashara iliyopo mkiani kwa soka iliyoonyesha mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima kwa aina ya soka walillocheza wageni hao.

Kipindi cha pili mabadiliko yaliyofanywa na kocha wa Biashara ya kuwatoa, George Makanga na Godfrey Mapunda na kuwaingiza, Mpapi Nassib na Kauswa Bernard, huku Yanga ikimtoa Thabani Kamusoko na Feisal Salum na kuwaingiza Amissi Tambwe na Pius Buswita.

Mabadiliko hayo ya Zahera yaliwabeba kutokana na kuwasoma Biashara waliojazana nyuma kulinda bao lao na Zahera kuwaingiza washambuliaji kuweza kuufungua ukuta huo.

Mabadiliko hayo yalimbeba Zahera na kufanikiwa kusawazisha bao huku kipa wa timu Biashara akichanwa usoni na kulazimika kufungwa bandeji kulinda jeraha lake.

Ndipo wakati Biashara wakifikiria mambo yangeisha kwa sare dakika ya 80 Makambo alifunga bao kwa kuwapiga chenga safi mabeki wa Biashara na kumchambua kipa na kuifanya Yanga kurejea kileleni mwa msimamo ikifikisha alama 41 ikiishusha Azam iliyokalia kiti hicho kwa muda baada ya ushindi wake wa mabao 4-0 dhidi ya Mbao.

Azam ina pointi 39, huku Simba ikiwa nafasi ya tatu na alama zao 27 licha ya kuwa na mechi za viporo vitatu ili kulingana na wababe waliopo juu yake, huku Biashara ikiendelea kusalia mkiani ikiwa na alama 10 baada ya mechi 15.