Yaliyojiri A. Lyon vs Ndanda FC

PAZIA la Ligi Daraja la Kwanza (FDL) limefunguliwa rasmi jioni ya leo kwa mechi mbili jijini Dar es Salaam, Africn Lyon waliikaribisha Ndanda FC na kutoshana nguvu kwa kufungana bao 1-1, huku jijini Dodoma wenyeji Fountain Gate waliipasua Alliance kwa mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Jamhuri.

Fountain ni moja ya timu mpya zilizopanda ligi hiyo kutoka Daraja la Pili (SDL) na ushindi huo umeifanya waanze FDL wakikaa kileleni, akisikilizia timu nyingine nane za Kundi B zitakazocheza kesho Jumamosi na Jumapili kwenye mfululizo wa ligi hiyo.

Achana na kipigo ilichopewa Alliance ambao msuimu uliopita ilikuwa Ligi Kuu Bara kabla ya kushuka dakika za mwishoni, sambamba na Ndanda, Lipuli, Mbao na Singida United, jijini Dar es Salaam kulikuwa na utamu kwenye Uwanja wa Uhuru Lyon ikiwa nyumbani ililazimishwa sare na Ndanda kwa mabao yaliyowekwa kimiani na  Kassim Yusuph  kwa lile la wenyeji na Ndanda kusawazisha kupitia Hatibu Jofrey.

Mwanaspoti ambalo lilikuwa likishuhudia mechi hiyo linakuletea mambo matano ambayo yalijitokeza.

Mafaza Ndanda

Kikosi cha Ndanda kilianza na Mafaza (wachezaji wazoefu) watano waliowahi kucheza katika timu mbalimbali za Ligi Kuu Bara na kutamba kimataifa akiwamo Jerson Tegete, Mrisho Ngassa na Henry Joseph, huku ikiwa na wakali wazoefu kama kipa Hashim Mussa, Khemed Manzi na Daniel Joram.

Katika mafaza hao Henry Joseph ambaye ni nahodha ndio alionekana kufanya vizuri akicheza katika eneo la beki wa kati.

Mastraika bado

Timu zote mbili zilionekana kuwa na shida katika eneo la kumalizia kwani walitengeneza mashambulizi mengi kila mmoja alitumia moja.

Tegete na Hamad Mbumba ndio walionekana kuongoza safu ya ushambuliaji ya Ndanda na wote hawakuonekana kuwa na viwango vizuri kutokana na kushindwa kutumia nafasi za kufunga ambazo walipata.

Lyon wao safu ya ushambuliaji ilikuwa na Gadi Mussa na Kasim Khamis aliyefunga bao ambao nao hawakuwa vizuri

Maandalizi duni

Kwa ambavyo Ndanda na Lyon walicheza wachezaji wa timu zote mbili walionekana kukosa maandalizi ya kutosha kwani walikuwa wakicheza huku wakionyesha kuchoka.

Kuna baadhi ya wachezaji wa timu zote mbili walikuwa mpaka wanadondoka jambo ambalo lilionyesha kukosa maandalizi ya kutosha na utimamu wa miili yao.

 

Mbinu za makocha

Kocha wa Lyon, Nizar Khalfan alionekana kuanza na mfumo wa (4-3-3), wakati mpinzani wake kocha wa Ndanda, Ngawina Ngawina alianza na (3-5-2).

Nizar alionekana kufauli katika kipindi cha kwanza kucheza vizuri na kutengeneza nafasi za kufunga ambazo walishindwa kuzitumia.

Wakati katika kipindi cha pili ilikuwa tofauti kwa Ngawina kuonekana kufaulu kwa upande wake tofauti na kipindi cha kwanza.

 

Kazi bado wanayo

Kwa namna timu zote zilivyocheza leo ilionekana zote kuwa na viwango vya kawaida na kwa maana hiyo zinapaswa zijipange kwelikweli kwani ni wazi kazi wanayo kama wanataka kurejea kwenye Ligi Kuu Bara.

Ili waweze kufanya vizuri Lyon na Ndanda wanatakiwa kujiandaa na kufanya maandalizi ya kutosha ili kubadilika na kuboresha viwango vyao na kucheza katika ubora.

Makocha wa pande zote mbili walisema wamekubali matokeo na wanaenda kujipanga kwa mechi zao zijazo katika ligi hiyo inayoshirikisha timu 20 zilizopangwa kwenye makundi mawili kusaka nafasi mbili za kupanda Ligi Kuu kwa msimu wa 2021-2022 na pia kuepuka kushuka daraja kwani kila kundi zitashuka nne moja kwa moja.