Yahya Alghassani : Aibuliwa na Mutu anasifa za Rashford

Muktasari:

  • Yahya anasema alianza kucheza soka akiwa na kikosi cha vijana cha FC Shabab Al-Ahli Dubai kabla ya Septemba 21 mwaka jana Al-Wahda FC Abu Dhabi kumnasa.

UWEZO wake wa kutokea pembeni na wakati mwingine kucheza kama mshambuliaji wa kati, umewafanya Waarabu wa Asia kumuona Yahya Alghassani ni kama Rashford wao kwenye Ligi ya Falme za Kiarabu ambayo ni maarufu kama ‘UAE Gulf’.

Yahya wa Al-Wahda FC Abu Dhabi ni kinda wa Kitanzania aliyezaliwa Aprili 18, 1998 anayecheza soka la kulipwa katika Taifa la Falme za kiarabu.

Nyota huyo wa Kitanzania ni mototo wa Ally Said ambaye ni mzaliwa wa Zanzibar Mkoa wa Kaskazini Pemba. Wilaya ya Wete Kijiji cha Shenge Juu.

Nje ya Bongo imepata nafasi ya kuzungumza naye pamoja na familia yake kwa ujumla ambayo inafurahishwa kwa kupiga kwake hatua kwa kijana huyo ambaye amekuwa miongoni mwa wachezaji 10 chipukizi hatari kwenye taifa hilo.

Yahya alizaliwa na kukulia Falme za Kiarabu anakoishi na familia yake, anajiona kama kijana mwenye bahati ya kuwa na wazazi, ndugu ambao wamekuwa wakimuunga mkono kwenye uchezaji wake soka.

“Napenda sana mpira, hilo baba aliligundua tangu nikiwa mdogo na kuamua kunipeleka kwenye vituo vya soka ambavyo kwa kiasi kikubwa vimenisaidia kujua namna ya kucheza mpira na kufuata utaratibu wake,” anasema.

MAMBO YALIVYOANZA

Yahya anasema alianza kucheza soka akiwa na kikosi cha vijana cha FC Shabab Al-Ahli Dubai kabla ya Septemba 21 mwaka jana Al-Wahda FC Abu Dhabi kumnasa.

“Nilikuwa nikicheza mashindano mbalimbali ya vijana huku nikiwa na ndoto kuwa ipo siku nitacheza Ligi Kuu, nadhani haikupangwa niichezee FC Shabab Al-Ahli Dubai ndipo niliposajiliwa na Al-Wahda,” anasema.

MUTU ALIMUIBUA

Baada ya kujiunga na Al-Wahda FC Abu Dhabi, kinda huyo wa Kitanzania alikutana na mtukutu, Adrian Mutu aliyewahi kutamba enzi zake akiwa na klabu kadhaa kubwa barani Ulaya kama vile Chelsea ya Ligi Kuu England, Juventus, Fiorentina, Inter Milan na nyinginezo za kibao za Italia.

“Mutu amenifundisha nikiwa chini yake kwenye timu ya vijana alinisaidia mambo mengi ya ndani na nje ya uwanja ili niweze kuwa mwanasoka mkubwa kwa siku za usoni.

“Yeye alichangia kupanda kwa kiwango changu kwa haraka na mwishowe benchi la ufundi la kikosi cha kwanza ndani ya kipindi kifupi liliamua kunipandisha haraka kikosi cha kwanza,” anasema Yahya.

ALIVYOPATA SHAVU

Alivyopandishwa tu,Yahya anasema alipata shavu la Desemba 27 mwaka jana kwenye mchezo wake wa kwanza kuvaa jezi ya kikosi cha kwanza cha Al-Wahda FC Abu Dhabi na kufunga bao lake la kwanza la msimu.

“Nilipata nafasi ya kuanza na hapo nyuma tulitoka kucheza na sikuwa hata kwenye orodha ya wachezaji wa akiba, nilishukuru sana kuona kocha ameniamini, nilicheza kwa kufuata maelezo na bahati mbaya mwanzoni mwa kipindi cha kwanza nilionyeshwa kadi ya njano kwa kucheza rafu.

“Nilifunga bao la kwanza kwenye mchezo ule ambao tulishinda mabao 5-0 ilikuwa kipindi cha kwanza, sikucheza kwa dakika zote 90 mwishoni mwa kipindi cha pili kocha alinitoa,” anasema.

MKATABA MNONO

Kiwango cha winga huyo wa Kitanzania mwenye umri wa miaka 20, kiliwastua Al-Wahda FC Abu Dhabi na kuamua kumpiga kitanzi cha mkataba mnono utakaomalizika 2023.

“Nashukuru Mungu kwa kipindi kifupi nilianza kukubalika na nivyofunga bao langu la kwanza wakaanza kunifananisha na Marcus Rashford wa Manchester United. Tulikaa chini viongozi wakaamua kunipa ofa ya mkataba mpya,” anasema.

SOKA LA UARABUNI

“Soka lao ni kubwa sema wachezaji wengi wa bara hilo wamekuwa wakikimbilia Ulaya kwenye ligi kubwa ukilinganisha na kwingineko, hata mimi pia nina ndoto za kucheza huko,” anasema.

AITAKA TAIFA STARS

Mbali na kuwa na mpango wa kucheza soka la ushindani barani Ulaya, Yahya anasema amekuwa na shauku ya kutaka kulitumikia taifa lake la Tanzania.

“Natamani kuichezea Taifa Stars, mimi ni Mtanzania pamoja na kuwa nimezaliwa na kukulia huku ila ukweli utabaki kuwa hivyo na siwezi kuwa kigeugeu kwa taifa langu,” anasema.

Usikose toleo lijalo ili kupata uhondo wa namna ambavyo baba wa kijana huyo amekuwa akimsapoti.