Woodward akiri kweli kutosa usajili wa Jose Mourinho

Muktasari:

Mourinho alihisi kwamba hakupata sapoti ya kutosha akiwa Man United katika kuwasajili wachezaji aliokuwa akiwataka baada ya kumshindwa kumpatia beki wa kati Harry Maguire na kumsajilia mastaa Diogo Dalot, Fred na Lee Grant kwenye dirisha la majira ya kiangazi mwaka 2018.

MANCHESTER, ENGLAND . BOSI kubwa wa Manchester United, Ed Woodward amekiri kuzuia dili moja au mbili za usajili wa wachezaji aliowataka Jose Mourinho wakati alipokuwa kwenye kikosi hicho cha Old Trafford kabla ya kunasa dili la kuinoa Tottenham Hotspur kwa sasa.

Woodward, ambaye ni makamu mwenyekiti wa Man United alimfuta kazi Mourinho Desemba mwaka jana baada ya kuona timu haina mwendo mzuri licha ya timu kutumia karibu Pauni 400 milioni kusajili nyota wapya.

Mourinho alihisi kwamba hakupata sapoti ya kutosha akiwa Man United katika kuwasajili wachezaji aliokuwa akiwataka baada ya kumshindwa kumpatia beki wa kati Harry Maguire na kumsajilia mastaa Diogo Dalot, Fred na Lee Grant kwenye dirisha la majira ya kiangazi mwaka 2018.

Woodward alisema: “Ni kweki kwamba kulikuwa na tofauti kidogo katika makubaliano ya mchezaji mmoja au wawili hivi baina ya kocha na idara ya usajili. Wakati mwingine mimi ndiye ninayepaswa kusema hapana, kwa sababu ni jambo la kawaida kwa kocha wetu kupingana na hilo, lakini tumekuwa tukisikiliza ushauri pia kwenye kusajili.”

Mourinho alihitaji kufanya usajili wa beki wa kati akiwa Man United na aliwakosa Toby Alderweireld wa Tottenham, Diego Godin kutoka Atletico Madrid na Bayern Munich, Jerome Boateng kabla ya klabu hiyo kutumia Pauni 80 milioni kumnasa Maguire kwenye dirisha lililopita la majira ya kiangazi.

Mourinho alihitaji wachezaji wengi zaidi kutinga kwenye kikosi chake, lakini bosi wake hakuwa tayari kufanya hivyo katika dirisha la majira ya kiangazi la mwaka 2018 kabla ya kwenda kufukuzwa kazi ilipofika Desemba.

Mourinho aliwahi kusema: “Ningependa kupata wachezaji wawili zaidi. Sidhani kama nitapata hao wawili. Nadhani inanwezekana pia nikapata mchezaji mmoja tu. Nimeipa klabu yangu orodha ya majina matano miezi michache iliyopita.”

Kisha alisema: “Manchester United imeuza wachezaji ambao kamwe nisingewauza na kununua wachezaji ambao nisingewanunua. Di Maria, Chicharito, Danny Welbeck hawa hapa, nisingeweza.”

Mourinho akaishia kufutwa kazi huko Man United na wakati anaondoka timu hiyo ilikuwa nafasi ya tisa kwenye Ligi Kuu England, ikiwa imevuna pointi 17 katika mechi 13.

Kikosi hicho kwa sasa kipo chini ya Ole Gunnar Solskjaer na mambo si mazuri, huku beki wa zamani wa Liverpool, ambaye kwa sasa ni mchambuzi, Jamie Carragher amemwambia Woodward amchukue tu Mauricio Pochettino kwenye kuokoa jahazi huko Old Trafford.