Wenger: Hazard hazibi pengo la Ronaldo

Muktasari:

Kwenye kikosi hicho cha Los Blancos, Ronaldo alifunga mabao 450 katika mechi 438, lakini hadi sasa Hazard amefunga mara moja tu kwenye mechi sita.

MADRID, HISPANIA. ARSENE Wenger amefunguka haoni na wala haamini kama Eden Hazard ni mtu sahihi wa kwenda kuziba pengo la Cristiano Ronaldo huko Real Madrid.
Chelsea ilimpiga bei Hazard baada ya kubeba ubingwa wa Europa League kwa ada ya Pauni 88.5 milioni baada ya staa huyo wa Kibelgiji kuweka wazi kwamba asingesaini mkataba mpya wa kuendelea kukipiga kwenye kikosi hicho cha Stamford Bridge.
Kwenye kikosi hicho cha Los Blancos, Ronaldo alifunga mabao 450 katika mechi 438, lakini hadi sasa Hazard amefunga mara moja tu kwenye mechi sita.
Wakati wanakamilisha dili lake kwenye dirisha lililopita la majira ya kiangazi, Real Madrid iliamini imempata mtu wa kuja kuziba pengo la Ronaldo, aliyeamua kutimkia zake Juventus mwaka jana. Lakini, kuziba pengo la Mreno huyo huko Barnebeu si kitu rahisi, amewasaidia kushinda mataji mawili ya La Liga na manne ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Huko alikotoka kwenye kikosi cha Chelsea, Hazard alifunga mabao 110 katika mechi 352, jambo ambalo Wenger haamini kama buti za Ronaldo zitakwenda kumtosha mchezaji huyo kwa sababu si aina ya wale wenye uwezo wa kufunga zaidi ya mabao 30 kwa msimu.
“Ataisaidia, lakini hawezi kuziba pengo la Ronaldo kiukweli. Hawezi kufunga mabao 50 kwa mwaka, hivyo ndivyo soka inavyotazamwa kwa sasa," alisema Wenger na kuongeza: “Madrid inahitaji mfungaji mwingine wa mabao kwa sababu Karim Benzema amekuwa na umri wa miaka 32 sasa, anahitaji kuwa na kijana wa kuja kuchukua nafasi yake. Hazard yeye abaki na utofauti wake wa kutengeneza nafasi hasa kwenye mechi kubwa.”