Wema: Kupatana na Kajala moyo wangu bado

Friday August 7 2020

 

By Nasra Abdallah

SIKU chache baada ya mrembo Wema Sepetu kupatana na rafiki yake Aunt Ezekiel, mashabiki sasa wamtaka amgeukie na Kajala ambapo mwenyewe amefunguka kuhusu hilo.

Wema na Aunt walikuwa wamegombana kwa miezi kadhaa lakini jana Alhamisi Agosti 6, 2020 walionesha kuzika tofauti zao baada ya kupatanishwa kwenye mahojiano na kituo cha televisheni cha E-TV.

Akihojiwa leo Ijumaa Agosti 7, 2020 kwenye kituo cha Clouds tv, Wema amesema yeye kama binadamu kuna ugomvi mkubwa na mdogo, lakini kwa Kajala anauweka katika ugomvi mkubwa.

Kutokana na hilo, amesema hataki unafiki na hayupo tayari kwa sasa kupatana na Kajala isipokuwa anamuachia Mwenyezi Mungu.

“Kupatanishwa kwetu hakujaanza jana wala leo, hata Steve Nyerere alishajitahidi kutafuta suluhu kuhusu hilo, lakini hajafanikiwa hadi leo, hivyo katika hili naomba niachwe kwanza sipo tayari kwa sasa,” amesema Wema anayetesa na tamthiliya ya Karma kwa sasa.

Alipoulizwa kama ikatokea Kajala akahitaji wapatanishwe atakuwa yupo tayari, amesema hiyo ni yeye lakini kwa sasa aachwe kwanza.

Advertisement

Hata aliposomewa baadhi ya vifungu katika vitabu vya dini na mtangazaji, kuhusu umuhimu wa kusamehe aliyekukosea, amesema kwake haijampunguzia wala kumuongezea chochote kutokana na ugomvi wao.

Advertisement