Waziri Waitara azindua Copa Coca-Cola Umisseta Manyara

Muktasari:

  • Katika ngazi ya Kitaifa Copa Coca-Cola Umisseta itafanyikia Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara mwaka huu.

Manyara: Mashindano ya mwaka 2019 ya Copa Coca-Cola Umisseta yamezinduliwa rasmi mkoani Manyara kwenye Uwanja wa Kwaraa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mwita Waitara.

Uzinduzi huo lilihudhuriwa na maofisa mbalimbali wa Serikali, maofisa michezo, walimu na wanafunzi kutoka shule mbalimbali za sekondari mkoani Manyara.

Akizundua michezo hiyo mkoani Manyara, Waitara aliishukuru kampuni ya Coca-Cola kwa kuwezesha michezo ya Copa Coca-Cola Umisseta kuzinduliwa rasmi mkoani humo kwa mara ya kwanza huku akiwahimiza vijana wa Manyara kuthibitisha vipaji vyao dhidi ya mikoa mingine kupitia mashindano hayo.

“Ningependa kuwahimiza vijana wa mkoani hapa kuifanya hii michezo kuwa sehemu ya kujifunza zaidi na njia ya kuongeza ushiriki katika shughuli za nje ya masomo. Tofauti na siku za nyuma, Michezo siku hizi ni biashara yenye thamani kubwa, na kila mmoja wenu hapa anaweza kuwa shahidi ya hili," alisema Waziri Waitara.

Alibainisha kumbukumbu zinaonyesha idadi kubwa ya vijana mkoani Manyara wamefanikiwa katika michezo kupitia Copa Coca-Cola Umisseta.

Mwakilishi wa Bonite Bottlers mkoani Manyara, Samwel Bitalian alisema kupitia michezo hiyo, Coca-Cola imedhamiria kuwafika wanafunzi wengi nchini kadri iwezekanavyo ili kuwapa fursa ya kushiriki katika michezo hiyo na kuvumbua vipaji.

Katika udhamini wa mashindano hayo, Kampuni ya Coca-Cola itasambaza vifaa vya michezo zaidi ya 2000 katika shule za sekondari nchini.

Uzinduzi wa mashindano ya Copa Coca-Cola Umisseta, katika ngazi ya mkoa katika mkoa wa Manyara ni wa tano tangu kuanzishwa kwa michezo hiyo mkoani Dodoma kasha Tanga, Zanzibar na Mtwara.

Katika ngazi ya Kitaifa michezo hiyo itafanyikia Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara mwaka huu.