Wawa, Onyango wazua jambo simba

MABEKI wa kati wa Simba, Pascal Wawa na Joash Onyango wamezua jambo baada ya kubainika kombinesheni yao ndio kali na isiyoruhusu mabao kirahisi na kufanya wadau wamtahadharishe Kocha Sven Vandenbroeck kukomaa nao kama anataka kuwa salama Msimbazi.

Kombinesheni hiyo haijaruhusu bao lolote katika mechi tatu walizopangwa pamoja kati michezo sita, iliyocheza Simba hadi sasa katika Ligi Kuu Bara.

Katika mechi mbili za awali za Simba, Kocha Sven aliwaanzisha kwa pamoja, Kennedy Juma na Onyango dhidi ya Ihefu na kushinda 2-1 na ile ya sare ya 1-1 ilipovaana na Mtibwa Sugar, huku mchezo wao wa sita iliocharazwa 1-0 na Tanzania Prisons, Onyango alianzishwa na Erasto Nyoni.

Baada ya kuona mambo hayaendi sawa kwenye zile mechi mbili za awali, Svena aliamua kuwachezesha Wawa na Onyango dhidi ya Biashara United na kushinda 4-0, kisha wanakainyoa Gwambina kwa 3-0 kabla ya kushinda tena 4-0 dhidi ya JKT Tanzania.

Kwenye mchezo wao uliopita, Sven alimwanzisha Nyoni kabla ya kumuingiza Kennedy baada ya Wawa kuwa na dharura iliyomfanya asafiri kwenda kwao Ivory Coast na kulikosa pambano hilo dhidi ya Prisons.

WASIKIE WADAU

Mtendaji Mkuu wa zamani wa Bodi ya Ligi na Klabu ya Azam FC, Saad Kawemba alizungumzia juu ya ukuta wa Simba, akisema soka ni mchezo unaoendeshwa kwa namba, hivyo Wawa na Onyango ni mabeki wazuri lakini wanatakiwa wapatiwe warithi wao mapema.

“Simba wanahitaji beki wa kati anayeanzisha mashambulizi, Wawa na Onyango ni wazuri, ila umri wao unaenda na kinachofanyika sasa wanatumika ili timu ipate matokeo mazuri. Sven anatakiwa ahakikishe anatengeneza wachezaji wa kuziba nafasi zao ili wakosekana kusiwe na shida kama sasa,” alisema.

Naye nyota wa zamani wa kimataifa, Zamoyoni Mogella alisema Sven anatakiwa aanze kutengeneza kombinesheni nyingine mapema ili Simba isitetereka anapokosekana mmoja wa mabeki hao wa kikosi cha kwanza.

“Haina haja ya kusajili beki mwingine wakati Ame (Ibrahim) yupo pale, umri unamruhusu kucheza, anatakiwa apewe muda mwingi wa kucheza, ili kiwango chake kiwe juu Sven anatakiwa aanze kumuangalia,” alisema Mogella aliyewahi kung’ara na timu za Simba, Yanga, Volcano ya Kenya na Taifa Stars, huku Mchambuzi wa soka, Ally Mayay alisema Wawa na Onyango wameweza kufiti kutokana na wote kucheza kwa kupishana.

“Wanapocheza Wawa na Onyango wote wanakaba na kutulia, tofauti na Erasto, Kennedy wakicheza na Onyango hapo mmoja lazima awe anasimama.”

Mayay alisema njia pekee ya kufanya kwa Sven kuondoa tatizo la kumtegemea mchezaji mmoja ni kutengeneza kombinesheni nyingine zinazoweza kupatikana kupitia mechi za kirafiki.”