Watatu Simba kuikosa Lipuli

Friday February 14 2020

Simba, Ibrahim Ajibu, Miraji Athuman na Mzamiru Yassin,Uwanja wa Samora mjini Iringa,

 

By Thobias Sebastian

WACHEZAJI watatu wa Simba, Ibrahim Ajibu, Miraji Athuman na Mzamiru Yassin wataikosa mechi dhidi ya Lipuli itakayochezwa kesho Jumamosi Uwanja wa Samora mjini Iringa, kutokana na matatizo tofauti.

Ajibu ambaye alikosekana pia mchezo uliopita dhidi ya Mtibwa Sugar hatakuwa sehemu ya kikosi mechi hiyo kutokana na matatizo ya kifamilia.

Miraji na Yassin wao bado ni majeruhi na wataendelea kukaa nje ya uwanja kutokana na ratiba yao ya matibabu ilikuwa inawataka kuwa nje kwa wiki sita ambazo zinaelekea ukingoni na baada ya hapo daktari ataamua kulingana na uchunguzi wa mwisho utakaofanywa.
Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu alisema wachezaji wengine wote wapo fiti na chaguo lipo kwa kocha mkuu Sven Vandernbroeck  atakavyoamua kuwatumia.

"Wachezaji majeruhi katika timu ni wawili tu, Miraji  na Mzamiru ambao nao nadhani baada ya muda mfupi watakuwa fiti na kurejea uwanjani lakini kwa upande wa Ajibu iliomba ruhusa kutokana na kupata matatizo ya kifamilia," alisema Rweyemamu.

Advertisement