Washambuliaji Yanga wampasua kichwa kocha Eymael

Muktasari:

Yanga sasa ina mastraika wanne David Molinga kinara wa ufungaji akiwa na mabao saba, Ditram Nchimbi bao moja, Tariq Seif (1), Yikpe Gnamien (2).

Dar es Salaam.Kocha wa Yanga, Mbelgiji Luc Eymael amesema washambuliaji wamekuwa wakitengeneza nafasi nyingi za kufunga katika kila mechi, lakini wameshindwa kuzitumia.

Kocha Eymael alisema Yanga imekuwa ikitegeneza nafasi nyingi za kufunga kila mchezo ila washambuliaji wake wamekosa umakini katika umaliziaji.

"Kiukweli bado limekuwa tatizo hili kwa washambuliaji wangu kushindwa kufunga mabao katika kila nafasi za kufunga kati ya nyingi ambazo tunapata" alisema Mbelgiji huyo.

"Kama kanuni za Ligi Kuu Bara zingekuwa zinaruhusu kusajili mchezaji huru hata kama dirisha limefungwa mimi ningefanya hivyo kwa kusajili mchezaji mwingine na angekuwa mshambuliaji mwenye uwezo wa kufunga.

"Lakini kwa hali ilivyo na kanuni bado inaendelea kunibana nitawaelekeza na kuwapa mbinu nyingi hawa niliokuwa nao katika timu ili waweze kufanya vizuri," alisema.

"Kama wangekuwa wanatumia kufunga nafasi ambazo tunapata huenda timu yetu ingekuwa na mabao mengi zaidi chini yangu, lakini tunakwenda kulifanyia kazi hili maana makocha ndio kazi yetu," alisema Eymael.

Yanga sasa ina mastraika wanne David Molinga kinara wa ufungaji akiwa na mabao saba, Ditram Nchimbi bao moja, Tariq Seif (1), Yikpe Gnamien (2).