Watatu wapangua vikosi Yanga, Azam
Muktasari:
- Kaimu Kocha Mkuu wa Yanga, Abdihamid Moallin, na Kocha Mkuu wa Azam, Florent Ibenge, wote wamefanya mabadiliko hayo katika vikosi vyao vya kwanza vinavyopambana kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara inayopigwa New Amaan Complex, Zanzibar.
VIKOSI vya Yanga SC na Azam FC vinavyokutana leo vimeonyesha mabadiliko ya wachezaji matatu kila upande ikilinganishwa na vilivyocheza mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB Juni 21, 2026 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza
Kaimu Kocha Mkuu wa Yanga, Abdihamid Moallin, na Kocha Mkuu wa Azam, Florent Ibenge, wote wamefanya mabadiliko hayo katika vikosi vyao vya kwanza vinavyopambana kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara inayopigwa New Amaan Complex, Zanzibar.
Moallin amewapumzisha mabeki Kibwana Shomari na Chadrack Boka, huku nafasi zao zikichukuliwa na Yao Attohoula na Mohamed Hussein.
Aidha, kiungo Mudathir Yahya ameanzia benchi, huku mshambuliaji Laurindo Aurelio 'Depu' akipewa nafasi ya kuanza.
Kwa upande wa Azam iliyoshinda mechi ya nusu fainali kwa mabao 3-2, Ibenge amelazimika kumkosa Yoro Diaby ambaye anatumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyopewa katika mechi hiyo. Nafasi yake imechukuliwa na Lameck Lawi, aliyefunga bao baada ya kuingia akitokea benchi katika mchezo huo.
Mabadiliko mengine yamewahusisha viungo Ashrafu Kibeku na Yahya Zayd ambao leo wameanzia benchi, huku Zidane Sereri na Sadio Kanoute wakianza katika kikosi cha kwanza.
Mabadiliko hayo ni wazi yanalenga kila upande kufanya vizuri katika kusaka pointi tatu kipindi hiki cha kuelekea mwisho wa msimu.
Yanga inayoongoza msimamo kwa pointi 66, inahitaji kushinda ili kuendelea kukaa kileleni na kutetea taji lake kwani baada ya leo, itabakiwa na mechi mbili dhidi ya TRA United (nyumbani) na JKT Tanzania (ugenini).
Azam yenye pointi 58 ikishika nafasi ya tatu, nayo baada ya leo itasafiri kwenda Tanga kukabiliana na Coastal Union, kisha itarudi nyumbani kumalizia ligi dhidi ya Dodoma Jiji.
Kikosi cha Yanga; Djigui Diarra, Yao Attohoula, Mohamed Hussein, Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Bacca, Duke Abuya, Maxi Nzengeli, Prince Dube, Laurindo Depu, Allan Okello na Pacome Zouzoua.
Kikosi cha Azam; Zuber Foba, Lusajo Mwaikenda, Pascal Msindo, Lameck Lawi, Twalib Nuru, Himid Mao, Zidane Sereri, Sadio Kanoute, Jean-Jacques Ngita, Feisal Salum 'Fei Toto' na Idd Seleman 'Nado'.