Wanyama mbioni kumfuata Samatta Aston Villa

Muktasari:

Villa tayari imesajili wachezaji watatu akiwemo Samatta, lakini bado wanataka kusajili wachezaji wengine wawili bora ili kuimalisha kikosi chao kinachopigana kujiokoa na janga la kukwepa kushuka daraja.

London, England. Kiungo wa kimataifa wa Kenya, Victor Wanyama yuko mbioni kufuata nahodha Tanzania, Mbwana Samatta katika klabu ya Aston Villa.

Taarifa kutoka ndani ya klabu ya Aston Villa zinasema kiungo hiyo wa Tottenham yupo katika mpango wa kuondoka katika klabu yake baada ya kocha Jose Mourinho kuonyesha nia ya kutaka kumpunguza katika kikosi chake.

Villa tayari imesajili wachezaji watatu akiwemo Samatta, lakini bado wanataka kusajili wachezaji wengine wawili bora ili kuimalisha kikosi chao kinachopigana kujiokoa na janga la kukwepa kushuka daraja.

Suala hilo ndilo linalofanya klabu hiyo kuingia sokoni kutafuta wachezaji bora kwa ajili ya kujenga kikosi chao.

Kwa mujibu wa Daily Record, Villa inafuatilia kwa karibu suala la Wanyama ndani ya Spurs wakati huu dirisha la usajili likiwa linaelekea mwishoni.

Wanyama alianza kucheza soka katika Ligi Kuu Kenya akiwa na klabu za Nairobi City Stars na AFC Leopards.

Alijiunga na Helsingborg ya Sweden kwa majaribio akiwa na kaka yake Mcdonald Mariga Wanyama. Baada ya Mariga kujiunga na Parma, Victor alirudi nyumbani Kenya.

Wanyama alirejea tena Ulaya na kujiunga na klabu ya Ubelgiji ya Beerschot AC mwaka 2008. Kiwango chake alichokionyesha Beerschot, alifanikiwa kujiunga na Glasgow Celtic.