Wanariadha katika mtego wa Taifa

Dar es Salaam. Nani atatwaa ubingwa wa Taifa? Hicho ni kitendawili ambacho kitateguliwa na wanariadha nyota nchini ambao leo wataanza kibarua cha kuipigania mikoa yao kwenye mashindano ya Taifa.

Mashindano hayo yanayoshirikisha wanariadha zaidi ya 400 kutoka mikoa 28 yatafunguliwa leo na Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Hassan Abbas.

Wanariadha kutoka mikoa yote shiriki wamewasili Dar es Salaam tayari kwa mashindano hayo ya siku mbili yanayofanyika kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, chini ya usimamizi wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) na Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC).

Kivutio kikubwa kwenye mashindano hayo ni namna ambavyo nyota wa mchezo huo nchini watakavyotoana jasho na wale wanaochipukia.

Mikoa ya Arusha, Simiyu, Pwani, Manyara, Dar es Salaam na Zanzibar huenda ikapata ushindani zaidi kutokana na historia yao kwenye riadha hivi sasa, huku Simiyu ikiingia kwenye orodha hiyo kutokana na kuwa mkoa unaoongozwa na rais wa RT, Anthony Mtaka.

Nyota wa timu ya Taifa, Failuna Abdi, Gabriel Geay, Panga Joseph, Mathayo Soji, Fabiano Joseph Naasi na Paul Itambu ni miongoni mwa nyota wanaotarajiwa kuchuana kuipigania mikoa yao kwenye mashindano hayo.