WAMETISHA: Mastaa Zenji kama wote Jangwani

MABOSI wa Yanga juzi walimtambulisha beki wa kushoto, Muharami Issa ‘Marcelo’ waliyemsajili kwa mkataba wa miaka mitatu akitokea Malindi FC ya Zanzibar.

Kabla ya Yanga kumtangaza, Marcelo alitajwa kusainishwa mkataba Singida United, lakini mlezi wa klabu hiyo, Mwigulu Nchemba aliyeahidi kuwasajilia Yanga mchezaji mmoja, ndiye anayetajwa kumhamishia Jangwani kutimiza ahadi yake.

Achana na ishu ya usajili wake Jangwani, lakini unaambiwa kutua kwa beki huyo ambaye anaenda kuchukua nafasi ya Gadiel Michael aliyesajiliwa Simba kwa mkataba wa miaka miwili, lakini mabosi wa Msimbazi wanaficha kuepuka msala kama ule wa Hassan Kessy, kumezidi kunogesha ule utamu wa wachezaji wa Kizenji kukinukisha Yanga.

Ndio kama hujui ni kabla ya miaka ya 2000 iingie na wimbi wa nyota wa Zenji kutua Jangwani ni kwamba Yanga ilishawahi kutamba na wachezaji kutokea visiwani, akiwamo kipa Riffat Said Mohammed, moja ya makipa hodari waliyowahi kutokea nchini.

Riffat aliyekumbwa na mauti Mei 9, 2000 akiwa na miaka isiyozidi 32 tu, aliwahi kuzichezea pia Mlandege, Malindi, Miembeni kabla ya kuibuka Coastal Union na Yanga sambamba na kuichezea timu ya taifa, Taifa Stars.

Unaambiwa tangu apite Riffat kisha kuingia miaka ya 2000, Jangwani wamekuwa wakinasa majembe ya maana kutoka Zenji moja wapo akiwa ni beki kisiki na nahodha wa zamani, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ aliyetokea Malindi na kuja kuwa mhimili mkubwa Yanga.

Kuna mashabiki kadhaa wa Yanga walishtuka kuona Yanga wakifanya hivyo kutokana na kwamba wachezaji wengi kutoka kisiwani Zanzibar wanadaiwa kuwa ni legelege kwa aina ya mpira wanaocheza.

Hata hivyo, Cannavaro aliweza kulizima zengwe hilo kwa kuonyesha ukomavu katika ukabaji na kujitolea katika timu kiasi cha kuwafanya Yanga wamkabidhi unahodha.

Baada ya kuonyesha hayo ni kama alifungua milango kwa Wazanzibar wenzake Yanga, akiwamo Abdi Kassim ‘Babi’ aliyetua Jangwani mwaka 2007 akitokea Mtibwa Sugar na kukinukisha vya kutosha.

Makala hii inaonyesha wachezaji kutoka Visiwani Zanzibar jinsi ambavyo wanatembelea nyota ya Cannavaro baada ya kufanya vizuri katika kikosi hicho.

ABDALLA SHAIBU ‘NINJA’

Baada ya Cannavaro kutundika daruga misimu miwili iliyopita, jezi yake namba 23 aliikabidhi wa Abdallah Shaibu ‘Ninja’ ambaye uchezaji wake ni kama beki huyo aliyechangia kumpeleka Jangwani.

Ninja ameondoka Jangwani bure katika kipindi hiki cha uhamisho baada ya mkataba wake kumalizika na kutua LA Galaxy ya Ligi Kuu ya Marekani (MLS) atakakocheza kwa mkopo kutoka klabu moja ya Jamhuri ya Czech.

Ninja ameacha kumbukumbu nzuri Yanga kwa soka lake la nguvu na kukinukisha kwa misimu miwili.

SAID JUMA ‘MAKAPU’

Ni miongoni mwa wachezaji wasiokuwa na makeke katika kikosi cha Yanga, lakini uwezo wake ndio ulimfanya aendele kubaki kikosini hapo akiwa mmoja ya wachezaji kiraka.

Makapu alikuwa akipata nafasi ya kucheza katika kikosi kutokana na uwezo wake wa kucheza kama kiungo lakini pia kama beki wa kati, hali hiyo ilimfanya mpaka apate nafasi ya kucheza katika kikosi cha Zanzibar Heroes.

Hata hivyo, maisha yake katika kikosi cha Yanga yamekatishwa baada ya kocha Mwinyi Zahera kuamua kumkata na kumuondoa katika mipango yake.

HAJI MWINYI MNGWALI

Ukikutana naye kutokana na umbo lake unaweza ukasema anacheza nafasi ya beki wa kati kutokana na urefu wake alionao, lakini sivyo.

Bila shaka Yanga walilamba dume kwa Mwinyi kwani Tambwe akiwa katika ubora wake alikuwa akifunga magoli mengi kutumia krosi zinazotokea upande wa kushoto kwa Mwinyi Haji.

Hakuna shabiki ambaye alikuwa na wasiwasi kwa Mwinyi pindi anapokuwa na mpira mguuni kwani ana uwezo wa kupiga krosi akiwa hata katikati ya uwanja.

Lakini yote hayo Kocha Mwinyi Zahera amemkata katika kikosi hicho baada ya mkataba wake kumalizika na mpaka hivi sasa hana timu.

FEISAL SALUM ‘FEI TOTO’

Kiungo huyu aliwaingiza Yanga katika mtafaruku mkubwa baada ya kusaini Singida United asubuhi na mchana alionekana makao makuu ya Yanga akisaini.

Huu usajili ulitikisa vilivyo lakini mwishowe Singida walikubali na kumuacha kijana avae jezi ya Yanga.

Ni miongoni mwa viungo bora ambao wana uwezo wa kucheza kama kiungo mkabaji lakini pia kama mchezeshaji katika kikosi cha Yanga.

Alikuwa katika kikosi cha Taifa Stars kwenye AFCON 2019 nchini Misri.

MOHAMMED ISSA ‘BANKA’

Uwezo wake katika kumiliki mpira pamoja na kupiga pasi za uhakika bila shaka kila mmoja anajua hilo.

Akiwa na Mtibwa Sugar alionyesha uwezo katika kumiliki dimba la kati kiasi cha kuwatoa mate mabosi wa Yanga na kufanikiwa kunasa saini yake mwaka jana.

Licha ya kudaka saini yake mwaka walishindwa kumtumia kutokana na kifungo lakini mapema Februari mwaka huu alianza kuichezea timu hiyo na kila mmoja aliona kazi yake anapokuwa uwanjani.

ABDULAZIZ MAKAME

Huyu ndiye pacha wa Feisal walipokuwa katika kikosi cha Zanzibar Heroes, lakini msimu ujao watakuwa pamoja katika kikosi cha Yanga.

Ni pendekezo la Kocha Mwinyi Zahera baada ya kuona anahitaji kiungo mwingine wa kunyambulika.

Makame ana sifa za kunyambulika na uwezo mzuri wa kumiliki mpira na kwa sasa mashabiki wanasubiri kuona mambo yake sambamba na Fei.

MUHARAMI ISSA ‘MARCELO’

Baada ya beki Gadiel Michael kutikisa kiberiti Yanga, mabosi wa klabu hiyo fasta wakaumiza kichwa na kujua nani atakuwa mrithi.

Baada ya kuona hivyo wakanyanyua simu kwa Mwigulu Nchemba na kumchukua beki Muharami Issa kutoka Zanzibar aliyesajiliwa wiki iliyopita na Singida.

Kutua kwake na kujumuika na Wazenji wenzake kikosi Jangwani bila shaka mashabiki wa Yanga watakuwa na hamu ya kuona ‘mziki’ wao msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na Klabu Bingwa Afrika.