Wambura sasa ambana Karia kieleweke

Muktasari:

Michael Wambura amesema anataka kujadili na Rais Karia kuhusu kuelekea Mkutano Mkuu wa TFF, Uchaguzi Mdogo ambavyo vyote vitafanyika Februari 2 , mwakani  na mambo mengine ya maendeleo yanayohusu soka nchini.

SIKU chache tangu arejeshwe madarakani na mahakama Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Michael Wambura amembana bosi wake, Rais wa shirikisho hilo, Wallace Karia kwa kumuandikia barua na kumopa masharti kadhaa.
Wambura ameliambia Mwanaspoti kuwa, amemwandikia barua Karia ili wakutane na kujadili mambo mbalimbali ya soka na mbali na barua hiyo alisisitiza kama bosi wake atashindwa kuheshimu mahakama basi anashauri afanye jambo moja kati ya matatu.
Katika mahojiano maalumu, Wambura alisema amempa muda hadi wiki ijayo kujibu barua hiyo na akikaa kimya basi atafuata taratibu nyingine za kisheria kwa kurudi mahakamani kujulishwa kupuuzwa kwa amri waliyotoa dhidi yake na TFF.
Wambura alisema kikubwa anachotaka kujadili na Rais Karia ni kuelekea Mkutano Mkuu wa TFF, Uchaguzi Mdogo ambavyo vyote vitafanyika Februari 2 mwakani  na mambo mengine ya maendeleo ya soka nchini.
"Nilichaguliwa na wanachama, Mahakama Kuu ndio ilitoa hukumu ya kurejeshwa kwangu, maamuzi ya mwisho ya mahakama hakuna mtu wa kuyapinga ndivyo inavyotakiwa kufuatwa.
"Niliamua kupeleka mwenyewe nyaraka za hukumu TFF kwa vile mimi ndiye mhusika na inaruhusiwa si kwamba mahakama ndio yenye jukumu la kupeleka taarifa hizo, hii pia itanisaidia mimi kuwa na uhakika wa kujua kama wamepokea maana muda ukipita nitalazimika kurudi mahakamani na kuwaeleza kuwa nilipeleka ila hakuna hatua iliyochukuliwa.
"Hivyo hata Karia asipochukua hatua yoyote katika barua hiyo na muda ukipita basi nitarejea mahakamani kuomba wamkumbushe kitu anachopaswa kukifanya," alisema Wambura

MAMBO MATATU
Wambura alimshauri Karia kama ataona moyo wake hauna amani ya kufanyakazi naye kama Makamu wake, basi afanye mambo matatu.
"Rais atekeleze maamuzi ya mahakama hilo moja vinginevyo atasababisha matatizo makubwa. Pili, akiona kufanyakazi na mimi haiwezekani ama hatakuwa huru basi aende kwenye mkutano mkuu akayaseme hayo hao ndiyo watakaoamua maana ndio waamuzi wa mwisho.
"Tatu, kama hawezi vyote viwili hapo juu basi aitishe mkutano mkuu na kuwaomba waridhie kufanya uchaguzi mkuu maana yeye hataweza kujiuzulu, ili viongozi wachaguliwe upya kwa ajili ya faida ya soka na Taifa kwa ujumla," alisema Wambura.
Wambura alisisitiza, Rais Karia ni wakati wake kuhakikisha anaondosha migogoro isiyokuwa ya lazima ndani ya TFF inayoweza kusababisha mpasuko mkubwa ndani ya chama na wadau wa soka nchini.
"Binafsi nipo tayari kufanyakazi na Karia na sina tatizo lolote wala sijawahi kugombana naye, nilichaguliwa na wanachama hivyo sina sababu ya kujiuzulu wanachama ndiyo watakaoniondoa," alisema Wambura.