VIDEO: Wambura atua kwa kishindo TFF, akabidhi barua asepa

Muktasari:

  • Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania, Michael Wambura amepeleka barua ya kurejea katika ofisini baada ya kushinda kesi yake mahakamani

Dar es Salaam. Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Michael Wambura leo saa 5:30 asubuhi alilipelekea barua yake ya kurejeshwa ofisini na Mahakama Kuu makao kuu ya TFF.

Wambura alifungiwa kutojihusisha na masuala ya soka nchini baada ya kufungiwa na kamati ya Maadili ya TFF, lakini alipiga uamuzi huo kwenda mahakamani ili kupata haki yake.

Wambura alifika katika ofisi hizo akiwa na Wakili wake, Emmanuel Muga, ambapo aliingia ndani na kukabizi barua hiyo kisha akatoka na kuzungumza na wanahabari.

Wambura alisema jambo kubwa ambalo alikuwa analitaka ni kupokelewa kwa barua yake, ambapo alikiri barua hiyo imepokelewa na kusainiwa licha ya kwamba hakukuwa na viongozi wa juu ndani ya Shirikisho hilo.

"Barua nimeileta na imepokelewa hapa japokuwa kwamba hakukuwa na kiongozi wa juu, lakini imefika sehemu salama na kusainiwa, kwahiyo tayari wanatambua uwepo wangu kwa sababu nimeshawapa taarifa," alisema.

Aliongeza TFF kama hawapo tayari na uamuzi wa Mahakama wana haki ya kukata rufaa, lakini wakikaa kimya wanatakuwa wanadharau uamuzi wa mahakama.

Wambura alifunguka zaidi na kusema kwamba tayari ameanza kazi rasmi tangu tarehe 30 baada ya kupokea majibu kutoka mahakamani.

"Mahakama imeshanirejesha kazini tangu walipotoa uamuzi, pia mimi sikufuta umakamu bali nilifungiwa kujihusisha na mpira," alisema.

Aliongeza atamtafuta Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe na kuzungumza naye namna ambavyo sheria zimekuwa zikivunjwa ndani ya Shirikisho hilo.

Wakili wake, Emmanuel Muga alisema kesi yao ilikuwa ni kupinga kufungiwa maisha kwa mteja wake na siyo kupeleka kesi ya masuala ya soka.

"Hatujaupeleka mpira mahakamani na ndio maana mpira ulikuwa unaendelea kama kawaida, sisi kuna kanuni na sheria ambazo zilivunjwa ndio maana tukaenda mahakamani na baada ya mahakama kuangalia wameona wapi sheria zilipovunjwa na kutoa uamuzi," alisema Muga.