Wakipigwa wala msishangae

Saturday August 17 2019

 

By Mwandishi wetu

WALIOSEMA namba huwa hazidanganyi wala hawakukosea, kwani unaambiwa saa 1 usiku wa leo pazia la Ligi Kuu Bara msimu wa 2019-2020 litafunguliwa kwa pambano la Ngao ya Jamii kati ya Simba na Azam, lakini rekodi ya unyonge ikimtesa Kocha wa Azam Etienne Ndiayiragije dhidi ya Wekundu wa Msimbazi watakaovaana nao kwenye Uwanja wa Taifa.

Simba na Azam zitaumana kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam ikiwa ni pambano la pili kwao kukutana kwenye michuano hiyo iliyoasisiwa mwaka 2001 kabla ya kusimama na kurejeshwa tena mwaka 2009.

Katika mchezo wao wa kwanza kukutana mwaka 2012, Simba iliitandika Azam kwa mabao 3-2, hivyo kufanya pambano la kesho kuwa mtihani mzito kwa Wanalambalamba ambao inanolewa na Kocha Ndayiragije ambaye hana rekodi nzuri kwa Vijana wa Msimbazi.

Kwa misimu mitatu tangu Mrundi huyo atue nchini na kuanza kuifundisha Mbao FC kabla ya kuhamia KMC msimu uliopita, hajawahi kuonja ushindi wowote mbele ya Simba ni mechi moja tu Ndayiragije aliambulia sare, lakini mechi nyingine tano zote amechezea.

Akiwa Mbao kwa misimu miwili, Ndayiragije alikutana na Simba mara nne, huku akipoteza mechi tatu kwa kulala 1-0, 3-2 na 5-0, huku mchezo mmoja ukiisha kwa sare ya 2-2, lakini akiwa na KMC msimu uliopita kocha huyo mbele ya Simba amenyooshwa nje ndani kwa kufungwa mabao 2-1 kila mechi.

Kwa rekodi hizo za Ndayiragije na zile za Azam mbele ya Simba ni wazi kocha huyo na vijana wake watakuwa na kibarua kizito cha kupindua meza mbele ya Wekundu hao wanaofundishwa na Patrick Aussems ambaye msimu uliopita alimburuza Mrundi huyo.

Advertisement

Licha ya rekodi hizo, lakini soka ni mchezo wa maajabu na kwa namna vikosi vyote vilivyofanya usajili kuimarisha vikosi vyao kwa msimu huu ni wazi pambano la leo usiku litakuwa na upinzani, huku Azam ikitaka kulipa kisasi cha mwaka 2012 cha michuano hiyo.

Pia watataka kulipa kisasi cha msimu uliopita katika Ligi Kuu Bara kwa kufumuliwa mabao 3-1, huku Meddie Kagere akitupia mabao mawili na John Bocco, nahodha wa zamani wa Azam akifunga bao jingine na Frank Domayo alifunga la kufutia machozi la Azam.

Kocha huyo amesisitiza kuwa, rekodi za nyuma hazimshughulishi na akili yake ni kuona katika mechi ya kesho anapata matokeo mazuri licha ya kukiri Simba ni moja ya timu ngumu nchini.

Timu hizo pia zitatumia mechi hiyo kama maandalizi ya kuelekea mechi zao za marudiano za michuano ya kimataifa, Simba ikijiandaa kuialika UD Songo ya Msumbiji waliyotoka nayo suluhu katika Ligi ya Mabingwa Afrika na Azam ikitarajiwa kuipokea Fesil Kemena ya Ethiopia waliowatungua bao 1-0 ugenini katika Kombe la Shirikisho Afrika wikiendi iliyopita.

WASIKIE HAWA

Nyota wa zamani wa Boniface Pawasa amezungumzia mchezo huo akidai hautabiriki licha ya rekodi kuibeba Simba, kwani alisema timu zote zina nafasi sawa ya kushinda.

Pawasa alisema pia mechi hiyo ni kama maandalizi ya michuano ya kimataifa kwa timu hizo na pia itatoa fursa kwa makocha wote kuona upungufu wa vikosi vyao kabla ya michezo yao ya marudiano wikiendi ijayo.

Simba itarudiana na UD Songo ya Msumbiji wakati Azam itaikaribisha Fesil Kemena ya Ethiopia ambao waliwaumiza ugenini kwa bao 1-0.

‘’Simba, Azam na Yanga ndizo timu kubwa na zinaangaliwa na watu wengi kwenye Ligi Kuu Bara hata kupokezana kuchukua taji hili la Ngao ya Jamii, hivyo nadhani mchezo wa kesho (leo) utatoa taswira ya ushindani kwa msimu mpya wa Ligi Kuu Bara,” alisema.

Juu ya ushindani wa vikosi alisema timu zote zina nyota wa kuamua matokeo na kwamba mashabiki watapata burudani kabla ya kipute cha Ligi Kuu kuanza wiki ijayo.

Winga wa zamani wa Simba, Ulimboka Mwakingwe alisema mechi ya leo ina utamu wake hasa baada ya Azam juzi usiku kuinyoosha Namungo kwa mabao 8-1, huku Simba ikitoka kupata suluhu kwenye uwanja mgumu nchini Msumbiji dhidi ya UD Songo.

“Simba ina kazi kubwa ya kufanya kupitia mchezo huo na hasa katika kurekebisha makosa ya kikosi chake, lakini hata kwa Azam nayo inaweza kuwasaidia pia,” alisema.

Naye Sekilojo Chambua alisema itakuwa mechi ngumu kwa timu zote mbili kwa sababu ni mechi ya fainali na inatoa nafasi kwa timu zote mbili kutwaa ubingwa huo ambao upo mikononi mwa Simba baada ya kuuchukua msimu uliopita.

“Usajili uliofanywa na pande zote mbili Simba imefanya usajili mzuri tofauti na Azam lakini haimaanishi kuwa usajili huu uliofanywa ndio utawapa matokeo ya ushindi kwa urahisi hapana, bali timu ambayo imejiandaa na wachezaji wao kufanya kazi vizuri ndio naipa nafasi,” alisema.

“Ushindi wa mabao 8-1, ambao Azam wameupata kwa Namungo umeongeza motisha na kuwajenga saikolojia kuelekea katika mchezo na Simba tofauti na wangepoteza,” alisema Chambua.

Imeandikwa na Judith Fumbo, Stanlaus Kayombo na Brian Charles (TUDARCO)

Advertisement