Wakenya wamkalia kooni Migne

Thursday June 13 2019

 

By Fadhili Athuman

WAKENYA wameendelea kupoteza imani na Kocha wa Harambee Stars, Sebastien Migne, zikiwa zimesalia siku chache makala ya mwaka huu ya Afcon 2019 kuanza huko Misri.

Baada ya kutaja kikosi chake cha wachezaji 23, wanaoenda Cairo, Wakenya wengi wameonyesha kutoridhika na uchaguzi wa kocha huyo, hasa baada kumtema kiungo mshambuliaji Anthony Teddy Akumu na kiungo mshambuliaji Christopher Mbamba.

Mbali na Mbamba na Akumu, Migne pia aliwaacha Cliffton Miheso na Brian Mandela. Mandela na Mbamba wao wamelazimika kukaa pembeni kutokana na kuwa majeruhi huku Miheso na Akumu, wao wakishindwa kumridhisha Migne. 

Mandela anayeichezea klabu ya Maritzburg United ya Afrika Kusini, ambaye alikuwa beki tajika wa Stars, aliumia goti siku ya Jumatatu, baada ya mazoezi ya asubuhi, huku Mbamba yeye akishindwa kupona Jeraha lake la muda mrefu, alilopata kabla ya kuitwa kikosini.

Mwanaspoti ilipata fursa ya kuongea na baadhi ya mashabiki wa soka nchini, katika nyakati tofauti ambapo wengi walionekana kuhoji uwezo wa mfaransa huyo aliyeiongoza Kenya kufuzu fainali za Afcon kwa mara ya kwanza baada ya miaka 15, huku wengine wakishangaa kutemwa kwa Akumu.

Mwandishi wa Habari, Zachary Oguda, ambaye hivi karibuni alizindua kitabu cha ‘Away from Victory’ kinachozungumzia maendeleo na historia ya soka la Kenya, aliwataka wanaomzunguka kocha huyo, kumkumbusha kuhusu matumaini ya Wakenya kuelekea fainali hizo.

Advertisement

“Ni bora niwe muwazi katika hili, naamini wanaomzunguka Migne watamkumbusha, Wakenya hawajatumia milioni 250 kuwezesha timu hii, ili iende Misri kufungwa. Kinachoniuma ni kitendo cha kumbeba majeruhi Mbamba, wakati wanajua ni majeruhi, huku wakiwaacha nyota wetu wazuri nyumbani

“Christopher Mbamba, Anthony Akumu, Clifton Miheso na Brian Mandela, wametemwa huku Ovella Ochieng na Masoud Juma ambaye hana timu, wamechukuliwa pamoja na beki ‘mbovu’ Bernard Ochieng. tuombe Mungu Migne asituangushe huko Misri maana kwa uchaguzi hum, tumuachie tu Mungu,” alisema shabiki mwengine ambaye hakuta jina lake litajwe

Advertisement