Wageni walitumwa kutikisa nyavu VPL

Monday July 27 2020

 

By THOMAS NG'ITU

MASTRAIKA wa kigeni wa Simba, Azam na Yanga, Meddie Kagere, Obrey Chirwa na David Molinga ndiyo waliofunika kwa upachikaji wa mabao katika msimu wa Ligi Kuu Bara uliomalizika jana Jumapili.

Pamoja na kwamba Kagere ameshindwa kuifikia rekodi yake ya mwaka juzi alipofunga mabao 23 msimu uliopita amefunga mabao 22 lakini ameisaidia timu yake ya Simba kutwaa taji la ligi kwa miaka mitatu mfululizo ikimaliza na pointi 88.

Chirwa anayekipiga Azam amefunga mabao 12 lakini timu yake imeshika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 70. Yanga na Azam sasa wanaomba dua ili Tanzania ipate uwakilishi wa timu nne kwenye michuano ya kimataifa ya Afrika.

Molinga raia wa Congo anayeichezea Yanga, amefunga mabao 11 licha ya kutoanza mara kwa mara katika kikosi cha kwanza ambapo amechangia kwa kiasi kikubwa kuisaidia timu yake kumaliza msimu huo ikiwa na pointi 72.

Yanga imeshika nafasi hiyo baada ya kuifunga Lipuli bao 1-0 katika mchezo wa mwisho wa ligi uliochezwa Uwanja wa Samora mjini Iringa.

Nyota wa Namungo, Blaise Bigirimana raia wa Burundi amefunga mabao 11 sawa na Molinga ambapo ameisaidia timu yake kumaliza nafasi ya nne msimu wa ligi uliopita.

Advertisement

Mbali na nafasi hiyo kwenye ligi, Namungo imetinga hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) ambapo watacheza na Simba kwenye Uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga.

Endapo CAF watatoa nafasi hizo basi Yanga itashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na Simba huku Azam watashiriki Kombe la Shirikisho na Namungo. Bigirimana amewahi kuzichezea Stand United pamoja na Alliance FC.

Mchambuzi wa soka nchini ambaye ana taaluma ya ukocha. Kenny Mwaisabula amesema viwango vya wachezaji hao ni vizuri, lakini Kagere amezungukwa na wachezaji wazuri wengi anaocheza nao kama Francis Kahata na Clatous Chama.

"Unajua kufanya vizuri inatokana na timu husika uliyopo, tumeona kabisa kwamba Kagere amezungukwa na watu wengi wenye ubora, hata ukimchukua Molinga ukimpeleka pale anakuwa bora zaidi,"

"Molinga hajapata nafasi ya kucheza mara kwa mara lakini ameonyesha wazi kwamba kazi ya ushambuliaji ni kufunga na amekuwa akifanya hivyo kwahiyo ni jambo bora,".

Ameongeza kwa kusema "Molinga pia ameonyesha utofauti wa wachezaji wazawa ambao wanapata nafasi ya kucheza lakini wanashindwa kufanya kazi zao vizuri,"

Nyota hao wanne wamefunga jumla ya mabao 56 katika msimu wa 2019-20.

Advertisement