Wadau wa ngumi:OBFT, TPBRC haijamtendea haki Mwangata

Thursday June 13 2019

 

By Imani Makongoro

Dar es Salaam.Wadau wa ngumi nchini wameilishukia Shirikisho la Ngumi za Wazi (OBFT) na Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa (TPBRC) wakidai wasimamizi hao hawakuutendea haki msiba wa aliyekuwa bondia na kocha wa ngumi nchini, Benjamin Mwangata.

Mwangata atazikwa Leo nyumbani kwao Mtwara, aliagwa jana jijini Dar es Salaam huku wasifu wake katika michezo ukishindwa kuelezwa katika ibada ya kuaga mwili wake licha ya nafasi hiyo kutolewa kanisani.

Mbali na wasifu wa Mwangata katika michezo kukosekana, vigogo wa TPBRC na OBFT walishindwa kushiriki katika kuaga mwili wa bondia huyo aliyetwaa medali ya fedha kwenye michezo ya Afrika ya 1987.

"Kwa rekodi ya Mwangata kwenye michezo na namna ambavyo ameagwa ni tofauti, tulitarajia kuwaona mabondia wengi waliopitia mikononi mwake lakini haikuwa hivyo, hata viongozi wajuu wa OBFT na hata TPBRC hatuwaoni," alisema mmoja wa wadau wa mchezo huo.

Mdau mwingine alisema hata wasifu wa Mwangata katika michezo haukusomwa, zaidi ya familia kueleza tu kwamba alikuwa mwanamichezo, jambo ambalo OBFT ilipaswa kuwa imejipanga kwenye hilo, lakini ilikuwa tofauti.

Katika wasifu wa Mwangata, kaka wa Marehemu Magnus alisema alizaliwa 1966 na kuwa mwanamichezo tangu 1983 na kuajiliwa na Jeshi la Wananchi, ameacha mjane na watoto watatu, kitendo ambacho kiliibua mijadara kwa wadau wa ngumi.

Advertisement

Viongozi wa OBFT waliohudhulia msiba huo alikuwa Andrew Mhoja (Makamu wa rais) na Riadha Kimweri (Mjumbe) ambao walikiri kuwepo kwa changamoto hiyo, huku wakiahidi kuliwasilisha kwenye kikao cha kamati ya utendaji kwa ajili ya kuanza kuwaenzi mabondia walioiletea nchi sifa.

Ngumi za kulipwa ambapo Mwangata pia amewahi kuwa kocha wa mabondia mbalimbali wa ngumi za kulipwa, hakuna kiongozi wa kamati ya Utendaji inayoongozwa na Joe Anea, Yahya Pori na Agha Peter aliyeshiriki katika msiba huo.

Bondia pekee wa kulipwa, Mada Maugo aliyeudhulia msibani alisema bado kuna tatizo la ushirikiano kwa mabondia nchini.

Mabondia wengine waliojitokeza kuaga mwili wa Mwangata ni Kameda Anthony, George Sabuni, Hamad Furahisha, Mazimbu Ally, Maneno Omary, Koba Kimanga na Chris Mutta.

 

Advertisement