Wachezaji wamtibua Kocha Man United

Friday April 26 2019

 

MANCHESTER, ENGLAND.OLE Gunnar Solskjaer amewaambia wachezaji wake bayana kwamba mchezaji mwenye mtazamo chanya na Manchester United ndiye atakayebaki kwenye kikosi hicho msimu ujao.

Kocha huyo ametoa kauli hiyo yenye kutishia nafasi za watu baada ya kukumbwa na kichapo  kutoka kwa Manchester City kikiwa ni cha saba katika mechi tisa za karibuni.

Mabao ya kipindi cha pili kutoka kwa Bernardo Silva na Leroy Sane yalitosha kuiweka Man United pagumu kwenye mpango wao wa kuwamo kwenye Top Four ili kukamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Solskjaer, aliyekuwa ameshinda mechi 14 kati ya 19 kipindi alichokuwa kwa muda, lakini amechapwa mara tano katika mechi saba za ligi tangu alipochaguliwa kuwa kocha wa kudumu na jambo hilo linaonyesha kazi ngumu inayomkabili katika kukijenga upya kikosi hicho.

Nahodha wa zamani wa Man United, Roy Keane waliwatolea uvuvi wachezaji wa timu hiyo kwamba watamwangusha Ole kama walivyofanya kwa Jose Mourinho.

Solskjaer alipoulizwa kuhusu kauli ya Keane, alisema staa huyo yupo sahihi kwa sababu ana uchungu mkubwa na Man United.

Ole alisema: “Huu si wakati wa kunyoosheana vidole, lakini wachezaji wanapaswa kufahamu majukumu yao kwenye kuichezea Man United."

Advertisement

Mechi ilizobakiza Man United kwenye Ligi Kuu England msimu huu watacheza dhidi ya Chelsea, Huddersfield na Cardiff City.

 

Advertisement