Wababe Ulaya vitani tena

Muktasari:

Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp alionekana mwenye furaha wakati akikwea pipa na jeshi lake kwenda kumkabili Frank Lampard na Chelsea yake.

Istanbul, Uturuki . MTOTO hatumwi dukani unaambiwa na leo ndio mwisho wa ubishi kwa wababe wa soka la Ulaya, Chelsea na Liverpool.

Shughuli ni kwenye kuwania taji la Super Cup, ambapo Chelsea waliobeba kombe la Europa watavaana na Liverpool ambao ndio mabingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Tayari vikosi vyote vimewasili jijini hapa mapema tu jana kwa mtanange huo huku Liverpool wakionekana kuwa na mzuka zaidi kutokana na ushindi wa mabao 4-1 kwenye mechi yao ya kwanza ya ufunguzi wa Ligi Kuu England dhidi ya Norwich City.

Pia, itakuwa inaingia kwenye Uwanja wa Vodafone Park ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kupindua matokeo mwaka 2005 walipoichapa AC Milan kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na kubeba taji hilo.

Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp alionekana mwenye furaha wakati akikwea pipa na jeshi lake kwenda kumkabili Frank Lampard na Chelsea yake.

Mastaa wake akiwemo Jordan Henderson, Sadio Mane, Mo Salah na Robert Firmino walionekana kuwa fiti kwa mchezo huo.

Hata hivyo, Liverpool haitakuwa na kipa wake namba moja, Alisson kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya kifundo cha mguu.

Kwa upande wake, Chelsea ambao wametoka kupewa kipigo kikali cha mabao 4-0 na Manchester United pale Old Trafford, wametua na moja kwa moja wakaingia mitaani kupata hewa na kujiweka sawa kisaikolojia.

Licha ya kupoteza mchezo wa kwanza mbele ya Man United, mastaa wa Chelsea walionekana kuwa na sura za furaha na wapo tayari kwa mpambano na jeshi la Klopp.