Waarabu kuwang’oa Kagere na Chama

Muktasari:

Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori alipoulizwa kuhusiana na ofa iliyopo mezani ikimtaka Kagere, alikiri kufanya mawasiliano ya simu na klabu mbili za Uarabuni zikihitaji saini ya straika huyo.

TAARIFA za straika matata wa Simba, Meddie Kagere kutakiwa na vigogo vya soka barani Afrika, zimezidi kupamba moto na mabosi wa Simba wameamua kuweka msimamo mkali.

Huu ni msimu wa kwanza kwa Kagere kuichezea Simba akitokea Gor Mahia ya Kenya ambako alitwaa tuzo ya mfungaji bora mara mbili mfululilzo na sasa ndiye anayeongoza kwa mabao Ligi Kuu Bara akiwa ametupia mabao 23.

Kwa muda mrefu Kagere amekuwa akihusishwa kwenda kukipiga na Zamalek ya Ligi Kuu ya Misri, lakini kumekuwa na ukimya katika usajili huo kutokana na mkataba wake ndani ya Simba.

Kagere alitua Simba kwa mkataba wa miaka miwili na sasa ametumikia mmoja.

Taarifa ambazo Mwanaspoti limezipata ni kuwa, Waarabu hao waliweka mezani dau la Sh700 milioni, lakini uongozi wa Simba ulikaa kimya na Zamalek imetua tena ikitaka huduma ya nyota huyo. Mwanaspoti linafahamu kwamba Zamalek imetenga dau la Sh 900 milioni kwa ajili ya saini ya Mnywarwanda huyo mwenye asili ya Uganda.

Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori alipoulizwa kuhusiana na ofa iliyopo mezani ikimtaka Kagere, alikiri kufanya mawasiliano ya simu na klabu mbili za Uarabuni zikihitaji saini ya straika huyo.

Mbali na Kagere, Magori alifichua kuna ofa nyingine ambayo inamtaka kiungo fundi wa mpira, Mzambia Clatuos Chama.

“Kweli tumekuwa tukipokea simu nyingi za kuhitaji wachezaji wetu hawa, lakini hakuna barua rasmi iliyofika mpaka sasa. Kama ikifika ofa nzuri, basi tutakaa kujadili na kutoa uamuzi sahihi,” alisema Magori.

Hata hivyo, Magori alisema Simba inahitaji kuendelea kuwa na wachezaji wa viwango vya juu waliopo kikosini kwao kwa sasa, lakini kama ofa zinakuwa tamu, basi lolote linaweza kutokea.

“Tulifanya usajili mzuri ndio maana unaona wachezaji wetu wanahitajika, sisi tunahitaji pesa ya maana ili tufanye usajili mzuri na tishio.

“Wachezaji wengi wamehusishwa kuhitajika na baadhi ya timu, lakini tunasubiri barua ndipo tufanye majadiliano,” alisema.

Kwa upande wake, Meneja wa Kagere, Patrick Gakumba alipoulizwa kuhusiana na ofa za Waarabu hao alisema kwa kifupi: “Ndio”

Naye Kagere alipoulizwa alikiri kutambua ofa za kuhitaji huduma yake zilizotolewa na timu za Kiarabu, lakini akasema jukumu hilo liko chini ya meneja wake ambaye ndiye anayefahamu, lakini yeye kazi yake ni kucheza.

MO amtuliza Mkude

Baada ya kiungo wa Simba, Jonas Mkude kuhusishwa kwenda kumalizana na moja ya klabu za hapa nchini, jana Alhamisi, Mwenyekiti wa Bodi ya Simba, Mohamed Dewji ‘MO Dewji’ alifanya kweli baada ya kumbakiza kikosini kiungo huyo.

Mkude ni miongoni mwa wachezaji ambao ni zao la Simba akianzia timu ya vijana na hadi sasa amekuwa katika ubora wa hali ya juu huku akiwa ni mchezaji anayependwa na wanachama pamoja na mashabiki wa klabu hiyo.

Jana Alhamisi, katika ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Instagram wa tajiri huyo (Mo Dewji) aliwashusha presha mashabiki wa Simba ambao walidhani Mkude msimu ujao atavaa uzi wa rangi ya timu pinzani.

MO Dewji alituma ujumbe ulioambatana na picha akiwa na Mkude wakiwa wanapeana mikono na taarifa hiyo imezima uvumi kuwa Mkude anakaribia kuondoka klabuni hapo.

Licha ya Simba kutamka kuwa itafanya usajili wa nguvu lakini mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara mara mbili mfululizo bado hawajaweka wazi wachezaji watakaowaacha na wale watakaobaki nao msimu ujao wa ligi.

Mara kadhaa mchezaji huyo anapomaliza mkataba wake huhusishwa na timu pinzani, lakini mabosi wake hufanikiwa kumbakiza kikosini.

SEVILLA YAISUKA SIMBA

Wakati Simba ikisubiri kupokea ofa zaidi kwa maandishi juu ya nyota wake hao, imeelezwa mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi Sevilla inayoshiriki Ligi Kuu Hispania imetumika kutambua upungufu wa kikosi cha Wekundu hao wa Msimbazi.

Mechi hiyo ilichezwa juzi Alhamisi na Simba ilifungwa mabao 5-4, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Simba, Sweddy Mkwabi alisema timu yao ilicheza vizuri tofauti na ilivyotarajiwa kwani, wapinzani wao wako daraja la juu kabisa barani Ulaya.

“Tumejifunza mambo mengi kutoka Sevilla, machache ambayo tumeyaona kutoka kwao kwanza ni kufanya usajili mzuri na imara kipindi cha usajili ili kuwa na timu bora kutokana na upungufu tuliouona,” alisema Mkwabi.

Hata hivyo, Mkwabi aliwaomba mashabiki wao kujitokeza kwa wingi katika mchezo wa leo Jumamosi dhidi ya Biashara United ambayo itakuwa siku rasmi ya kukabidhiwa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Alisema mechi na sherehe zao za ubingwa bila mashabiki ni kazi bure hivyo wamepunguza kiingilio ambacho kitakuwa Sh 3000 kwa kila mtazamaji na mgeni rasmi wa mchezo huo ni Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola.

“Mechi itaanza saa 9 alasiri ili kutoa nafasi hata wale walio katika kipindi cha mfungo kuwahi kufuturu na ndio maana tumeshusha kiingilio, ni matumaini yetu mashabiki hawatatuangusha,” alisema.

MSIKIE AUSSEMS

Kocha wa Simba, Patrick Aussems alisema hakufikiria matokeo ya ushindi katika mechi dhidi ya Sevilla kwani anatambua walikuwa wanacheza mchezo na timu kubwa duniani ambayo imepiga hatua ndani na nje ya uwanja.

“Malengo yetu yalikuwa ni kucheza soka la kuvutia ili kila mchezaji apate nafasi ya kucheza na kuandika historia.

“Msimu huu kila mchezaji alikuwa nguzo muhimu kufanikisha ubingwa ambao tulibeba msimu uliopita, kwa maana hiyo ilikuwa vyema kila mchezaji kupata nafasi ya kucheza kwa kuheshimu kile ambacho amekifanya,” alisema.