Waamuzi wa Ligi Kuu England walivyogawana timu za kushabikia

Monday April 15 2019

 

LONDON, ENGLAND.WAAMUZI wa soka siku zote wanapaswa kutokuwa na upande wowote wanapokuwa uwanjani kuchezesha mechi, lakini jambo hilo halina maana kwamba hawana timu wanazozishabikia.

Kwa sababu nao ni binadamu kama walivyo binadamu wengine ndio maana wanakuwa na uhuru wa kushangilia timu za soka zinazowapendeza.

Kwenye Ligi Kuu England kuna marefa kibao waliofichuliwa timu zao wanazoshabikia, lakini jambo zuri ni kwamba hakuna hata mmoja aliyekiri kushabikia moja ya timu zinazoshika nafasi sita za juu kwa maana ya Liverpool, Manchester City, Tottenham, Chelsea, Arsenal na Manchester United.

Martin Atkinson– Leeds United

Mwamuzi huyo aliyezaliwa Machi 31, 1971 huko katika mji wa Bradford ameripotiwa kuishabikia timu ya Leeds United. Kwenye Ligi Kuu England alianza kuchezesha mechi mwaka 2005, huku mechi zake kubwa alizowahi kuchezea ni pamoja na ile fainali ya Kombe la FA ya mwaka 2011 iliyozikutanisha Manchester City na Stoke City.

Mechi nyingine ni fainali ya Kombe la Ligi baina ya Manchester United na Sunderland mwaka 2014. Atkinson ni mwamuzi wa beji ya Fifa alianza kwa kuwa mwamuzi msaidizi mwaka 1998 kabla ya kuanza kupuliza kipyenga kwenye Ligi Kuu England Aprili 2005.

Advertisement

Michael Oliver– Newcastle United

Michael Oliver ni moja ya waamuzi maarufu kabisa kwenye Ligi Kuu England kwa sasa. Mzaliwa huyo wa mji wa Ashington, alijiunga kwenye Ligi Kuu England mwaka 2010 huku timu yake anayoshabikia ni Newcastle United inayonolewa na Mhispaniola, Rafa Benitez.

Mechi zake kubwa baadhi alizowahi kuchezea ni pamoja na fainali ya Kombe la FA mwaka 2018, ambapo Chelsea waliichapa Manchester United 1-0 na ile pia ya Kombe la Ligi 2016, wakati Man City iliposhinda kwa penalti dhidi ya Liverpool kwenye mchezo wa fainali. Alikamatia filimbi pia kwenye kipute cha Ngao ya Jamii 2014, wakati Arsenal ilipokandamiza Man City 3-0. Oliver naye ni mwamuzi mwenye beji ya Fifa na amekuwa akichezesha pia mechi kadhaa za Ligi ya Mabingwa Ulaya na mechi za kimataifa.

Jon Moss– Sunderland

Mwamuzi, Jon Moss ni mmoja kati ya wale wenye heshima kubwa wanaochezesha Ligi Kuu England. Mwamuzi huyo ameripotiwa kuwa shabiki wa Sunderland. Alizaliwa Oktoba 18, 1970 katika mji wa Sunderland na ndio maana haishangazi kuona akiwa shabiki wa timu hiyo. Kwenye Ligi Kuu England alijiunga mwaka 2011 na moja ya mechi zake kubwa alizowahi kuchezesha ni ile fainali ya Kombe la FA mwaka 2015, wakati Arsenal walipoichapa Aston Villa 4-0.

Moss alianzia kucheza soka la chini sana kabla ya kupandishwa daraja na kucheza mechi za ligi. Huku nyuma alikuwa mwalimu wa shule na moja ya wanafunzi wake alikuwa kiungo wa Liverpool, James Milner.

Andre Marriner– Aston Villa

Moja ya waamuzi wakongwe waliopo kwenye Ligi Kuu England kwa sasa, akiwa amejiunga na ligi hiyo kuchezesha mechi zake mwaka 2005. Marriner alizaliwa Novemba Mosi, 1971 katika mji wa Birmingham na ameripotiwa kuwa shabiki wa timu ya Aston Villa.

Moja ya mechi kubwa alizowahi kuchezesha kocha huyo ni fainali ya Kombe la FA 2013, ambapo Wigan Athletic waliiduwaza Manchester City kwa kushinda 1-0.

Mechi yake ya kwanza kuchezesha kwenye ligi ilikuwa baina ya Charlton Athletic na Norwich City mwaka 2005. Mwamuzi huyo amekuwa akichezesha pia mechi za Europa League na michuano ya kufuzu kwa mikikimikiki ya ubingwa wa Ulaya.

Anthony Taylor– Altrincham

Mwamuzi, Anthony Taylor amekuwa na bahati sana ya kuchaguliwa kucheza mechi kubwa kwenye Ligi Kuu England. Refa huyo alizaliwa Oktoba 20, 1978 huko jijini Manchester na ameanza kujiunga na Ligi Kuu England tangu mwaka 2010. Timu inayotajwa kushabikiwa na refa huyo ni Altrincham.

Moja ya mechi kubwa alizowahi kuchezesha ni ile fainali ya Kombe la FA mwaka 2017, ambapo Arsenal waliichapa Chelsea 2-1 na ile fainali ya Kombe la Ligi 2015 ambapo Chelsea walijipigia Tottenham Hotspur Mbili Bila. Kwa miaka minane alikuwa akichezesha ligi za mchangani, miaka minne kwenye Football league, kabla ya kuingia kwenye Ligi Kuu England na kupewa pia nafasi ya kushika filimbi kwenye mechi kubwa huko England.

Mike Dean– Tranmere Rovers

Moja ya waamuzi wenye umri mkubwa kwenye Ligi Kuu England akizaliwa Juni 2, 1968 huko kwenye mji wa Wirral na amejiunga kwenye ligi hiyo mwaka 2000. Mwamuzi huyo, ambaye moja ya mechi zake kubwa zilizoacha kumbukumbu alizowahi kuchezesha ni ile ya fainali ya Kombe la Ligi 2011, ambapo Arsenal waliduwazwa na Birmingham kwa kuchapwa 2-1. Timu anayoshabikia Mike Dean ni Tranmere Rovers. Ndani ya mwezi huu, Mike Dean aliweka rekodi kwenye Ligi Kuu England kwa kuonyesha kadi nyekundu 100, wakati alipomntoa beki wa Manchester United, Ashley Young kwenye mechi ya kichapo dhidi ya Wolves.

Craig Pawson– Sheffield United

Craig Pawson alianza kuchezesha mechi za Ligi Kuu England mwaka 2013 na tangu wakati huo amekuwa mmoja wa waamuzi mahiri kabisa kwenye ligi hiyo, huku moja ya mechi zake kubwa kuchezesha ilikuwa nusu fainali ya Kombe la FA mwaka 2017, wakati Arsenal walipoichapa Manchester City 2-1.

Pawson, aliyezaliwa katika mji wa Sheffield mechi yake ya kwanza kuchezesha kwenye Ligi Kuu England ilikuwa baina ya Swansea City na Newcastle mwaka 2013.

Kabla ya hapo, refa Pawson alikuwa akichezesha kwenye ligi za chini ikiwamo ile ya mchujo ya League 2 baina ya Crewe na Cheltenham.

Kevin Friend– Leicester City

Mwamuzi, Kevin Friend alizaliwa Julai 6, 1971 katika jiji la London na aliingia kwenye Ligi Kuu England mwaka 2009 na ameripotiwa kuishabikia timu Leicester City.

Moja ya mechi zake kubwa alizowahi kuchezesha ni ile ya Ngao ya Jamii 2012, wakati Chelsea ilipokubali kipigo cha 3-1 kutoka kwa Manchester City.

Mwamuzi huyo alianza kwa kuchezesha mechi nyingi cha mchangani kabla ya kuibukia kwenye Ligi Kuu England huku mechi zake nyingine kubwa kuchezesha ilikuwa kwenye nusu fainali ya Kombe la Ligi mwaka 2008 iliyozikutanisha Hull City na Watford.

Lee Mason– Bolton Wanderers

Lee Mason ni mwamuzi mwenye uzoefu zaidi kwenye Ligi Kuu England. Alianza kuchezesha ligi hiyo siku nyingi na alizaliwa kwenye mji wa Bolton na ndio maana haishangazi kuona ni shabiki wa Bolton Wanderers.

Amechezesha mechi nyingi zenye umuhimu kubwa ikiwamo ile ya zile za mchojo wa kupanda daraja huku zile mechi zenye ushindani mkubwa kwenye mikikimikiki ya Kombe la Ligi. Alichezesha mechi mbili za mchujo kwenye Championship, ikiwa ni vipute muhimu vya kusaka timu za kupanda Ligi Kuu.

Chris Kavanagh– ameficha

Mwamuzi, Chris Kavanagh ni moja kati ya wenye umri mdogo wanaochezesha Ligi Kuu England baada ya kuzaliwa mwaka 1985.

Mwamuzi huyo alizaliwa kwenye jiji la Manchester na amegoma kuweka wazi timu yake anayoshabikia. Kwenye Ligi Kuu England, Kavanagh alianza kuchezesha mwaka 2017, ambapo alishika filimbi katika mchezo baina ya West Brom na Southampton.

Kwenye jiji la Manchester, timu maarufu zinazotoka katika eneo hilo ni Manchester United na Manchester City, lakini mwamuzi huyo amegoma kusema anashabiki timu gani.

Waamuzi wengine

Mwamuzi Roger East, alijiunga na Ligi Kuu England mwaka 2013, huku akishindwa kuweka bayana timu yake anayoshabiki, wakati Graham Scott, amefichua kuishabiki Swindon.

Mwamuzi Stuart Attwell ametangaza kuishabiki Luton Town, wakati Paul Tierney ni shabiki mkubwa wa Wigan.

David Coote amegoma kutaja timu yake anayoshabikia wakati Simon Hooper amefichua kuwa shabiki mkubwa wa Timu ya Swindon na amekua akiifuatilia kiala mara na anafurahi inapopata matokeo mazuri uwanjani.

Advertisement