WINO MWEUSI : Stars kujikwaa sio kuanguka,amkeni mpambane

Muktasari:

Stars baada ya kujikwaa katika Afcon, wanatakiwa kutambua kujikwaa si kudondoka kwa maana ya kushibdwa kufanya vizuri Afcon, basi kupambana kufa na kupona katika mechi ya kufuzu CHAN, dhidi ya Kenya.

WAKATI nasoma Shule ya Msingi Gilmani Rutihinda iliyopo jijini Dar es Salaam, niliwahi kufundishwa na mwalimu wangu wa Kiswahili, kujikwaa si kuanguka.

Kwa kipindi hicho, msemo huu niliuona kama wa kawaida tu kwa kuzingatia kujikwaa si lazima udondoke.

Hata hivyo, baada ya kuendelea na vidato hadi namaliza masomo yangu ya chuo kikuu, nimekuja kufahamu maana nyingi tu za misemo ukiwamo huu wa Kujikwaa sio kuanguka.

Nikafahamu maana yake, unaweza ukakutana na kikwazo katika maisha yako, lakini isiwe sababu ya kushindwa kuendelea kufanya vizuri katika jambo ambalo umekusudia.

Achana na hilo turudi hapa Tanzania katika kikosi cha timu ya Taifa “Taifa Stars” wakishindwa kufanya vizuri katika kombe la Mataifa Afrika (Afcon), nchini Misri kwa kufungwa mechi zote za hatua ya makundi na kuishia hapo.

Baada ya hapo timu ilirudi nchini na siku chache baadaye walikuwa na mechi za kufuzu fainali za CHAN, kucheza dhidi ya Kenya hapa nyumbani.

Hapa ndio nilikumbuka msemo wa kujikwaa si kuanguka kwa maana ya Stars kushindwa kufanya vizuri kwenye Afcon, si jambo la kukata tamaa kutoka tulikuwa na sababu nyingi ambazo zilichangia kuvuna ambacho tulipanda kama ambavyo wino mweusi wa Jumatano iliyopita ilieleza.

Stars baada ya kujikwaa katika Afcon, wanatakiwa kutambua kujikwaa si kudondoka kwa maana ya kushibdwa kufanya vizuri Afcon, basi kupambana kufa na kupona katika mechi ya kufuzu CHAN, dhidi ya Kenya.

Wepenzi wengi wa soka waliamini hilo linaweza kufanikiwa kwani kabla ya mchezo na Kenya, Satrs ilifanyiwa maboresho katika benchi la ufundi kwa kuachana na kocha mkuu Emmanuel Amunike na kuchukuliwa Mrundi Ettienne Ndayiragije pamoja na wasaidizi wake Selemani Matola na Juma Mgunda.

Mashabiki walimini Stars inakwenda kufanya vizuri katika mechi ya Kenya baada ya kuitwa katika kikosi wale wachezaji vipenzi vya mashabiki ambao walikosekana mara kwa mara katika kikosi hiko kilipokuwa chini ya Amunike.

Katika mechi ya kwanza ambayo Stars walikuwa nyumbani siku ya Jumapili uwanja wa Taifa dhidi ya Kenya mchezo huo ulimalizika kwa suluhu matokeo ambayo mashabiki wengi hawakutegemea kuona hivyo.

Wino mweusi wiki hii, inawakumbusha wachezaji na mashabiki Stars kuwa kushindwa kufanya vizuri kwenye Afcon na hata mechi ya kwanza ya kufuzu CHAN, dhidi ya Kenya ni sawa na kujikwaa.

Wachezaji na mashabiki wanachotakiwa ni kufahamu wakati huu wamejikwaa kwenye Afcon na CHAN, ila wananafasi ya kutokuanguka katika mechi ya marudiano na Kenya ambayo itachezwa Agosti 4, Uwanja wa Kasarani Nairobi.

Katika mchezo huo mashabiki waliokuwa na uwezo wa kwenda Kenya kuipa nguvu Taifa Stars ni jambo muhimu kwani shabiki ni mchezaji wa 12, hata wale mashabiki wa mpira ambao wanaishi nchini humu si mbaya wakafika uwanjani nao kufanya hivyo.

Kama wachezaji wakaweza kupambana zaidi ya mechi ya kwanza kuna kila sababu ya kupata ushindi au hata sare ya mabao ambayo itawafanya Stars kusonga katika hatua inayofata.

Nawakumbusha tu mashabiki kujikwaa katika mechi ya kwanza na Kenya si kuanguka kama wataweza kujitokeza katika mechi ya pili watawaongeza nguvu na morali ya kushindana wachezaji na wakafanya jambo kubwa la kuweka historia kwenda katika hatua ya pili kucheza na Sudan baada ya kuwatoa nishai Kenya nyumbani kwao.

Hautakuwa mchezo rahisi kwa kikosi cha Stars ila wanatakiwa kupambana na kuwafanya wapenzi wa soka waache kukata tamaa na kuamini kweli kujikwaa si kuanguka haswa katika kuhitaji kufikia malengo yako.

Wino mweusi inawapa hongera pia wandishi wa habari ‘Waandamizi’ katika kuhamasisha mashabiki kwenda kwa wingi Kenya kama vile ambavyo walifanya hapa Dar es Salaam, katika mechi ya kwanza kwani hamasa yao hiyo iliwaingia wachezaji, makocha na viongozi wa Stars.