WINO MWEUSI : Tanzanite Queens imetusuta mchana kweupe

Thursday August 15 2019

 

By Thobias Sebastian

WIKI tatu nyuma zilizopita kikosi cha timu ya Taifa ya Wanawake chini ya miaka 20, Tanzaniate Queens, kilikuwa katika maandalizi ya michuano ya Shirikisho la soka Kusini mwa Afrika (Cosafa), kama wageni waalikwa ambao yalikuwa yakifanyika Afrika Kusini.

Kikosi hicho cha Tanzanite Queens, chini ya makocha Bakari Shime na Edna Lima walioita wachezaji zaidi ya 25 ambao walifanyiwa mchujo ndani ya wiki moja na kubaki 20 - ambao ndio walikwenda katika mashindano.

Kipindi chote ambacho walikuwa wakifanya maandalizi ya mashindano hayo kulikuwa na mwamko wa kawaida kwa viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), waandishi wa habari na wadau wengine mbalimbali.

Mwamko ambao Wino Mweusi wiki hii unauzungumzia ni ule ambao kama timu ya Taifa ya waanaume ‘Taifa Stars’ inapokuwa inaitwa kwa ajili ya mchezo wa kirafiki au wa mashindano kwani Tanzania nzima huwa inafahamu.

Kimsingi na ukweli ambao haupingiki katika timu za Taifa ambazo zinapata nguvu ya kutosha katika maeneo yote ni Taifa Stars, ambayo mbali ya muda mwingi kushindwa kupata matokeo kama yale ambayo yanafikiliwa na Watanzania wengi, lakini inapata nguvu ya kutosha.

Taifa Stars huwa wanapata nguvu kwa viongozi wa TFF, kwa kuwa mbali ya kukutana nao mara kwa mara kwa kuwapa maneno ya kuwahamasisha kulingana na mechi husika, lakini wamekuwa wakipishana kwenda kuwatembelea mazoezini.

Advertisement

Nguvu nyingine ambayo Stars wanaipata wanapokuwa kambini wanakuwa katika hoteli nzuri ya maana kuliko zile ambazo wanakaa timu za taifa nyinginezo ambazo muda mwingi hukaa katika hosteli za TFF.

Katika maslahi, kwa maana posho za kila siku nazo ndio usiseme, lakini hata upande wa waandishi wenzangu wa habari tumekuwa mstari wa mbele kufanya kila tunaloweza katika kikosi cha Stars na kusahau timu nyingine jambo ambalo si sahihi.

Achana na hilo la Stars kabla ya Tanzanite Queens kutusuta mchana kweupe, kikosi cha timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys, nao walialikwa katika mashindano ya Cosafa ambayo yalifanyika mwaka 2018 nchini Botswana na kuondoka mabingwa wa mashindano hayo kwa kuwafunga Angola katika mechi ya fainali.

Serengeti Boys wao walikuwa katika maandalizi ya Kombe la Mataifa Afrika ambayo yalifanyika hapa nyumbani na licha ya kushindwa kufanya vizuri, lakini waliitoa nchi kifua mbele katika Cosafa, baada ya kuwa mabingwa mbali ya kualikwa katika mashindano hayo.

Ukiangalia na kufuatilia kwa karibu hata Serengeti Boys hawakupata nguvu na motisha ya kutosha wakati wanakwenda katika mashindano hayo kama vile ambavyo Stars ilipata wakati ilipokuwa inakwenda kwenda Afcon nchini Misri.

Tuachane na hayo, turudi hapa sasa kwa Tanzanite Queens ambao ni wazi wametusuta mchana kweupe na kutuachia somo la kujifunza baada ya kutoka katika mashindano hayo ya Cosafa yaliyofanyika huko Afrika Kusini.

Tanzanite Queens kwa muda waliokuwa hapa kambini si rahisi kuwepo katika hoteli yenye hadhi kama ambayo walikuwepo Stars. Pia si rahisi kupata posho na vifaa vya mazoezi kama vile ambavyo ilikuwa kwa Stars.

Mpaka wanaondoka hapa nchini waandishi wa habari wengi walikuwa hawawafuatilii na kuuhabarisha umma wa Watanzania hasa wale wapenda michezo kuhusu maendeleo ya timu hiyo na hata ilivyokuwa kule Afrika Kusini kwenye mashindano.

Viongozi wa TFF, mbali ya baadhi yao kuungana na timu hiyo kuna somo kubwa la kujifunza kwa Tanzanite Queens kwa kile ambacho wamekwenda kukifanya katika mashindano hayo ili kuwa na mwendelezo wa kufanya hivyo katika mashindano mengine.

Somo lingine ambalo TFF wanatakiwa kujifunza kwa wachezaji hawa wa Tanzanite Queens ni kuwatunza na kuwaweka pamoja ili kuja kucheza katika timu ya Twiga Stars ambayo nayo imekuwa ikipata matunda katika baadhi ya mashindano ingawa imekuwa haipati nguvu kama ile ya Stars.

Yote kwa yote Tanzanite Queens baada ya kuiwakilisha nchini vizuri katika mashindano hayo na kutwaa ubingwa kulionekana kuwapo na mwamko mkubwa kwa waandishi na baadhi ya wadau kujitokeza Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa wa Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam kuwapokea, jambo ambalo linaweza kuwa kama msoto kwetu kutokana walivyoondoka haikuwa hivyo.

Tanzanite Queens ilipokewa kwa shangwe la aina yake, lakini hata muda ambao walikuwa hawajafika pale uwanja wa ndege kulikuwa tayari kuna waandishi wa habari na wadau ambao walikuwa wamewasili kwa ajili yao.

Wino mweusi unawakumbusha kuwa Tanzanite Queens wametusuta kwa hili, na tunatakiwa kuangalia wadau wote wa soka kwa kila ambaye anahusika kwa nafasi yake kutimiza jukumu lake ili kuepuka aibu kama iliyotokea.

Huenda Tanzanite Queens isingefanikiwa kutwaa ubingwa wa mashindano hayo wangerudi kimyakimya kama vile ambavyo waliondoka na hakuna hata angeonyesha kujali walau kuwapongeza kwa kuonyesha ukomavu wa kushiriki mashindano makubwa dhidi ya nchi zilizoendelea katika soka.

Kikubwa hili ambalo walimefanya Tanzanite Queens linatakiwa kuwa fundisho kwa kila ambaye anahusika katika soka la nchini. Hii bila kujali ni timu yetu ya Taifa na kila mmoja ana jukumu la kuhakikisha inapasa sapoti ya kutosha.

Wino mweusi unapenda kuwapongeza wachezaji, benchi la ufundi na kila ambaye alikuwa sehemu ya kufanikisha Tanzanite Queens kuchukua ubingwa huo na kuifanya nchi yetu kuingia katika rekodi kwenye soka la wanawake.

Advertisement