WALE MAKINDA MATATA ULAYA WANAPOCHUANA

Sunday October 18 2020

 

LONDON, ENGLAND. ENGLAND imeingiza makinda watano, Jadon Sancho, Mason Greenwood, Bukayo Saka, Callum Hudson-Odoi na Phil Foden kwenye orodha ya wakali 20 wanaowania tuzo ya Golden Boy kwa mwaka huu wa 2020.

Makinda hao watano wote walikuwa kwenye viwango bora kabisa walipozitumikia klabu zao kwa msimu wa 2019-20 na sasa wote wamejumuishwa kwenye kikosi cha wakubwa cha timu ya taifa ya nchi hiyo, Three Lions.

Tuzo hiyo, inayotolewa na Tuttosport, inawahusu wachezaji wote waliozaliwa Januari 1, 2000 na kuendelea, ambao wanacheza kwenye ligi kubwa za Ulaya, ambapo waandishi wa habari 40 watapiga kura kupata washindi waliocheza soka la juu zaidi kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Baada ya orodha ya awali iliyohusisha wachezaji 100 iliyotangazwa Juni, kumefanyika mchujo mara nne wa kuondoa wachezaji 20 na hivyo kubakiza wachezaji 20 ambao ndio wametinga fainali kwenye mchakato huo.

Sancho alizidiwa na Joao Felix mwaka jana, lakini anaamini kiwango chake bora kabisa alichokionyesha Borussia Dortmund kinampa nafasi nzuri ya kutamba mwaka huu.

Greenwood anatarajia kuweka rekodi ya kuwa kinda wa nne wa Manchester United kushinda tuzo hiyo ya Golden Boy. Makinda wengine wa miamba hiyo ya Old Trafford waliowahi kushinda tuzo hiyo ni Wayne Rooney (2004), Anderson (2008) na Anthony Martial (2015).

Advertisement

Staa mwenzake Sancho huko Erling Haaland naye anatarajia kufuata nyayo za Mario Gotze za kubeba tuzo hiyo akiwa kwenye kikosi hicho cha miamba ya Bundesliga.

Kinda mwingine wa Kingereza kwenye tuzo hizo ni Saka, ambaye ameonyesha mambo makubwa kwenye kikosi cha Arsenal, hasa kwenye michuano ya Europa League.

Hudson-Odoi alicheza mechi 33 kwenye kikosi cha Chelsea msimu uliopita licha ya kuwa majeruhi na ubora wake wa uwanjani uliifanya miamba ya Ujerumani, Bayern Munich kupiga hesabu za kunasa huduma yake.

Na kinda mwingine, Foden amepenya kwenye kikosi cha Manchester City huku kiwango chake bora kikimpa nafasi katika timu ya taifa ya England. Foden, aliyepachikwa jina la Iniesta mpya, alifunga mabao matano katika mechi za kumalizia msimu kufuatia janga la corona na msimu huu tayari ameshafunga mara mbili.

Hata hivyo, staa anayetishia wengi kwenye tuzo hiyo ya mwaka huu ni Haaland, ambaye alifunga mabao 44 katika mechi 40 alizocheza msimu uliopita akiwa na kikosi cha Red Bull Salzburg na Borussia Dortmund.

Hivi karibuni alifunga hat-trick yake ya kwanza kwenye soka la kimataifa na hivyo kumfanya awe amefunga mabao 11 katika mechi 10 alizocheza hadi sasa msimu huu.

Kwingineko, miamba ya La Liga, Barcelona na Real Madrid kila moja imeingiza makinda mawili kwenye tuzo hizo.

Fati, ambaye atafikisha umri wa miaka 18 mwishoni mwa mwezi huu, aliibukia kwa kasi kubwa huko Nou Camp msimu uliopita na amemzidi Lionel Messi kwa mabao alipokuwa na umri kama wake.

Kinda huyo matata kabisa ameshaichezea na kufunga akiwa na timu ya taifa ya wakubwa ya Hispania na bado anaonyesha makali ya hali ya juu kwenye La Liga na Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kwenye kinyang’anyiro hicho ataungana na mchezaji mwenzake, Sergino Dest ambapo beki huyo wa kulia Mmarekani alitua Nou Camp katika majira haya ya kiangazi akitokea Ajax.

Huko Bernabeu, makinda wawili wa Kibrazili, Vincius na Rodrygo ndio walioingia kwenye orodha hiyo baada ya ubora wao wa soka kuisaidia Los Blancos kubeba ubingwa wa La Liga msimu uliopita.

Mshindi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Alphonso Davies naye ameingia kwenye kinyang’anyiro hicho kutokana na kiwango chake bora alichokionyesha akiwa na kikosi cha Bayern Munich, huku Mcanada mwanzake, Jonathan David naye akipenya kutokana na ubora alionyesha huko Gent, alikofunga mabao 23 msimu uliopita na kubamba dili la kwenda kujiunga na Lille ya Ufaransa.

Mastaa wapya wa Ligi Kuu England, Ferran Torres NA Fabio Silva, ambao wamejiunga Manchester City na Wolves mtawalia, walihitimisha robo ya wanaochuana kuwania tuzo hiyo kuwa ni wakali wanaocheza England.

Kinda wa Rennes, Eduardo Camavinga - anayehusishwa na Real Madrid na Manchester United mkali wa Paris Saint-Germain, Mitchel Bakker na Ryan Gravenberch wa Ajax ni wachezaji wengine kwenye orodha hiyo.

Juventus imemwingiza Dejan Kulusevski, RB Salzburg imemwingiza Dominik Szoboszlai na AC Milan imemwingiza Sandro Tonali kwenye orodha hiyo ambapo mshindi atatangazwa Desemba 14.

Advertisement