Viungo Mtibwa wampa Sven kazi nyingine

Muktasari:

Simba inarudi Dar es Salaam kucheza na Biashara katika Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumapili Septemba 27, 2020

Dar es Salaam. Simba imepoteza pointi mbili mapema katika Ligi Kuu Tanzania bara kwenye mchezo wao wa juzi dhidi ya Mtibwa Sugar uliofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.

Mabingwa watetezi, ambao walipewa nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi kwenye mchezo huo walijikuta wakipata sare ya bao 1-1 iliyosababishwa na mbinu ya Mtibwa.

Kiungo mshambuliaji, Mzamiru Yasin alianza kuiadhibu timu yake ya zamani kwa shuti kali akimpokonya mpira Baraka Majogoro kabla ya wenyeji kusawazisha kupitia kwa Boban Zirintusa kwa kichwa.

Simba, ambayo ilikuwa na nyota wake wote, ilishindwa kutamba katika eneo la kiungo, ambalo Mtibwa iliamua kuwavuruga mabingwa hao kwa kuwajazia wachezaji wengi eneo hilo.

Kocha Zuberi Katwila aliujua ubora wa Simba na kuamua kuwatumia Majorogo, Haruna Chanongo, Juma Nyangi na Jojo, huku akianza na mshambuliaji mmoja, Ibrahim Hamad ‘Hirika’.

Licha ya Kocha wa Simba, Sven Vandebroeck aliwaanzisha Jonas Mkude, Mzamiru Yasin, Clatous Chama, wakati pembeni wakiwa na Luis Miquissone na Benard Morrison, wakati mshambuliaji pekee akisimama John Bocco.

Ubora wa Mtibwa ulionekana katika kuzima mashambulizi ya winga hatari kwa sasa, Luis na Morrison, ambao walionekana wasumbufu, ambao walishindwa kupewa nafasi ya kuingia ndani ya eneo la hatari.

Uimara wa mabeki wa pembeni wa Mtibwa, Salum Kanoni na Issa Rashid ‘baba Ubaya’ ulikuwa msaada mkubwa kwa kikosi cha kocha Katwila katika muda wote wa mchezo.

Majogoro, ambaye ukiacha kosa la kusababisha bao lililotokana na kujiamini zaidi, alikuwa na maelewano mazuri na Juma Nyangi na Jojo, ambao walimrahisishia kazi Chanongo kusogeza timu juu.

Matarajio makubwa yalikuwa pembeni na hata kocha wa Simba, Sven aliamua kuwa na mchezo wa kasi kama ambavyo amezoea, lakini hakukuwa na njia katika maeneo yote.

Bocco alishindwa kuwa na msaada katika eneo la kati baada ya kuwa na wakati mgumu mbele ya Dickson Job na Luseke, ambao muda wote wa mchezo walikataa kufanya makosa kumruhusu nyota huyo wa zamani wa Azam FC kugeukia lango lao.

Inawezekana kuwa mabadiliko ya Simba ya kumwingiza Meddie Kagere yalichelewa zaidi kutokana na kuachwa kwa Bocco katika eneo la ushambuliaji, huku Chama aliyekuwa kama mshambuliaji mwingine nyuma yake akikosa ubunifu.

Hakuna shaka kwa Mtibwa kufurahia sare hiyo kutokana na kucheza na timu yenye ubora uwanjani kwa sasa, ikiwa pia na usajili wa nyota wapya walioongezwa kwa ajili ya mashindano ya Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kocha wa Mtibwa, Katwila alisema kupata sare dhidi ya Simba lilikuwa jambo gumu na limewapa motisha ya kufanya makubwa zaidi katika michezo yao ijayo ya Ligi Kuu.

Kauli hiyo inadhirisha ugumu alioupata Katwila katika kukabiliana na Simba na mpango alioingia nao katika mchezo ulikuwa na msaada kwao.

Mchambuzi wa soka, Ally Mayay alisema katika mchezo huo, lazima kikosi cha Mtibwa kipewe credit.

“Ubora wa Simba uko zaidi kwenye kiungo, hivyo Mtibwa ilihakikisha inawadhibiti Simba katika idara hiyo na wakafanikiwa,” alisema Mayay.

Alisema mpango wa Simba ilifeli, kwani walianza kwa kumuanzisha mshambuliaji mmoja na mawinga wawili wenye spidi.

“Kocha alitaka mawinga wale wamtengenezee nafasi John Bocco, lakini ikashindikana, na kocha alitegemea Chama na Mzamiri wazibe nafasi ya ushambuliaji.

“Lakini wakakutana na beki wa pembeni wa Mtibwa wenye spidi, hivyo wakawadhibiti ipasavyo Simba,” aliongeza kiungo huyo wa zamani wa Yanga.

Akizungumzia ubora wa safu ya ushambuliaji wa Simba, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Iddi Kipingu alisema kwa mechi mbili huwezi kuwahukumu nyota hao.

“Bado washambuliaji wake wapo vizuri na ndiyo timu iliyokuwa na safu bora ya ushambuliaji msimu uliopita, Bocco yupo vizuri, Kagere pia, hivyo bado safu yao ya ushambuliaji ipo imara,” alisema Kipingu.

Katika michezo ya mapema jana, Ihefu ilipata ushindi wake wa kwanza Ligi Kuu kwa kuichapa Ruvu Shooting kwa bao 1-0 lililofungwa na Enock Jiah.

Biashara United imeendeleza ubabe wake kwa kuichapa Mwadui bao 1-0 lililofungwa na Deogratius Mafie na kuifanya miamba hiyo ya Musoma kufikisha pointi sita.