Vita mpya ya Simba, TP Mazembe ipo hapa

Muktasari:

Kocha wa Simba, Patrick Aussems amekabana koo na mwenzake wa TP Mazembe, Pamphile Mihayo lakini Mbelgiji huyo akapigwa bao eneo moja tu.

SIMBA imeanza kupiga hesabu za michezo yao miwili ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe, ambao watakutana kwenye hatua ya robo fainali.

Ratiba inaonyesha Simba itaanzia nyumbani Aprili 6, mwaka huu, lakini kabla ya mechi hizo takwimu zinaonyesha mchezo huo utaamuliwa na vita ya makocha wakipishana kidogo kwa rekodi zao kwenye soka barani Afrika.

Kocha wa Simba, Patrick Aussems amekabana koo na mwenzake wa TP Mazembe, Pamphile Mihayo lakini Mbelgiji huyo akapigwa bao eneo moja tu.

Aussems Afrika

yuko Congo

Ukiondoa kufanya kazi kwa mafanikio nchini China, beki huyo wa zamani wa Standard de Liège ya Ubelgiji katika soka la Afrika ameweka rekodi zake tam utu akiwa pale Congo Brazzavile mwaka 2014.

Akiwa katika kikosi cha AC Leopards nchini humo, Aussems mafanikio yake makubwa yalikuwa kuifikisha timu hiyo hatua ya Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho.

Katika ajira yake ya mwaka mmoja akiwa hapo ramani yake ya mafanikio ilianza alipowang’oa Medeama ya Ghana kwa mikwaju ya penalti 5-4, baada ya timu zote kulingana kwa matokeo ambapo Leopards ilishinda nyumbani kwa mabao 2-0 kisha kukubali kipigo kama hicho ugenini.

Alipovuka hapo aliingia hatua ya makundi akiwa kundi A na kumaliza vinara wa kundi lao akifungana pointi na Cotton Sport ya Cameroon wakiwa wote na pointi 11, Aussems aliposhinda mechi 3, akitoa sare 2 na kupoteza moja.

Safari ya Auusems na Leopards yake iliishia hatua ya Nusu Fainali alipongolewa na Sewe Sport ya Ivory Coast kwa bao moja tu, akipoteza ugenini 1-0 kisha kutoa suluhu akiwa nyumbani.

Hata hivyo, Sewe nao walijikuta wakiangukia kuwa mshindi wa pili baada ya kupoteza katika fainali dhidi ya Al Ahly na kung’olewa na faida ya bao la ugenini, baada ya kushinda nyumbani 2-1 kisha kufungwa 1-0 matokeo yaliyowabeba Ahly kwa bao lao la ugenini.

Mfungaji bora wake

Aussems alifanikiwa kuacha historia baada ya kutoa mfungaji bora kwa straika wake Kader Bidimbou kuibuka kuwa mfungaji bora katika ligi hiyo akifikisha mabao 6.

Rekodi hiyo inaweza kumbeba Aussems kufuatia sasa akiwa Ligi ya Mabingwa hatua ya robo fainali, rekodi ya Bidimbou inakaribia kuwa katika himaya ya mshambuliaji wake mwingine Meddie Kagere mwenye mabao 6, akifuatiwa na kiungo Clatous Chama mwenye mabao 5.

Kabla ya Leopards, Aussems aliwahi kufanya kazi kwa miezi kadhaa nchini Sudan akiwa na kikosi cha Al Hilal aliofanikiwa kuwapa tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa, lakini pia timu hiyo ikiwa bingwa bila kupoteza mchezo wowote kisha baadaye kutibuana na mabosi wa timu hiyo na kutimka.

HUYU WA

MAZEMBE SASA

Wakati Aussems akiwa na rekodi hiyo mpinzani wake mpya wa sasa, Pamphile ameonekana kuwa mbishi baada ya kuwapa TP Mazembe kombe moja la Shirikisho katika kabati lao la makombe akifanya hivyo mwaka 2017.

Kiungo huyo mkongwe wa kikosi hicho safari yake ya msimu huo wa mafanikio kama kocha aliianza hatua ya mtoano alipowang’oa JS Kabylie ya Algeria kwa ushindi wa nyumbani kwa mabao 2-0 kisha ugenini kulazimisha suluhu.

Alipotinga hatua ya makundi Pamphile, ambaye alipewa jina la Baba na mashabiki wa Mazembe aliangukia kundi D na kumaliza kinara akiwa a pointi 12 akishinda tatu, sare tatu akiwa hajapoteza nafasi ya pili ilianguka kwa Super Sport ya Afrika Kusini waliokuwa na pointi 10.

Timu hizo mbili sasa ndiyo zilikuja kukutana hatua ya fainali, ambapo kuanzia hatua ya robo fainali Mazembe ya Pamphile ilishinda kwa kwa jumla ya mabao 7-1 dhidi ya Al-Ubayyid ya Sudan aliposhinda ugenini 2-1 kisha kupata ushindi mkubwa nyumbani kwa mabao 5-0.

Super Sport wao wakawang’oa Zesco robo fainali walitoa suluhu nyumbani kisha kupata sare ugenini ya mabao 2-2 a ‘Wasauzi’ wakivuka kwa faida ya bao la ugenini.

Nusu Fainali Mazembe ilikutana na FUS Rabata ya Morocco wakishinda kwa bao 1-0 nyumbani kisha ugenini wakilazimisha suluhu na kufanikiwa kutinga fainali huku Super Sport wao wakiwang’oa Club Africain ya Tunisia.

Fainali Mazembe iliandika historia ikichukua kombe hilo ikimchapa Super Sport jumla ya mabao 2-1 nyumbani kisha kulazimisha suluhu ugenini na kutwaa taji lake kubwa Afrika akiwa kama kocha.

Hata hivyo, Pamphile akiwa kama kiungo wa Mazembe ametwaa taji la Ligi ya Mabingwa mara mbili, 2009 na 2010 akiwa na Mazembe lakini pia akichukua Super Cup ya Caf mara moja 2010.

Ugenini wote

wachovu

Simba kufika hatua ya robo fainali inaumizwa na rekodi yao moja mbovu ya kutoshinda ugenini mechi nyingi, ambapo msimu huu imeshinda mechi moja tu dhidi ya Mbabane Swallows ya Swaziland kwa mabao 4-0, lakini kuanzia hapo haiajshinda tena mpaka sasa.

Aussems aliliambia Mwanaspoti kuwa hiyo ndiyo changamoto kubwa kwa sasa na wanataika kuifanyia kazi ili kufanya vizuri mbele ya Mazembe wakimaliza hatua ya makundi bila kufunga bao huku pia ikipoteza mechi tatu kwa jumla ya mabao 12.

Mazembe ikiwa chini ya Pamphile imepoteza mechi moja tu msimu huu ugenini ilipokubali kipigo cha mabao 3-0 dhidi ya Constantine ya Algeria, lakini pia ikitoa sare tatu zote ugenini.

Nyumbani kila mtu ashinde kwake

Simba ikiwa nyumbani haijapoteza katika hatua ya makundi na hata mtoano ikishinda mechi zote msimu huu ikiruhusu mabao matatu tu na ushindi mkubwa kwao nyumbani ni mabao 4-1 walipowachapa Mbabane.

Mazembe nao wakiwa nyumbani hutoki salama wakishinda mechi zote nne msimu huu na hakuna mpinzani aliyefunga bao timu hiyo ikiwa nyumbani msimu huu.