Viongozi Yanga zingatieni haya kuimarisha klabu ili mfanikiwe

Muktasari:

Timu zetu zikiwamo za Taifa ambazo kwa wakati mmoja zimewahi kuiwakilisha nchi kwenye mashindano mbalimbali zimepitia kipindi kigumu ambapo matokeo na matukio yaliyofuatia ndiyo yaliyotudhihirishia kuwa mambo hayakuwa sawa.

KWA muda sasa klabu ya soka ya Yanga inapita kwenye wakati mgumu, kutokana na hali ya mambo inavyoonekana, ambapo imekosa matokeo mazuri uwanjani kwa muda mrefu, licha ya kufanya usajili mkubwa na wa aina yake.

Licha ya usajili wa msimu huu, lakini huko nyuma msimu uliopita, vilevile ilijikuta kwenye wakati mgumu, ambapo hata katika juhudi zake za kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara hazikuzaa matunda.

Kwa sekta ya michezo nirahisi sana kubaini uwepo wa tatizo mahali popote, kwani hali hiyo huonekana tu kupitia matokeo yanayoonekana uwanjani pale timu au wanamichezo wanapokuwa wakicheza ambapo ama huishia kupoteza (kushindwa) au kugoma kuingia dimbani kucheza.

Ndivyo ilivyo katika tasnia hii. Waswahili husema mchezo hauchezwi gizani, ndio maana matokeo na matukio hushuhudiwa na kila mtu mwenye fursa ya kuona kinachoendelea.

Timu zetu zikiwamo za Taifa ambazo kwa wakati mmoja zimewahi kuiwakilisha nchi kwenye mashindano mbalimbali zimepitia kipindi kigumu ambapo matokeo na matukio yaliyofuatia ndiyo yaliyotudhihirishia kuwa mambo hayakuwa sawa.

Chukulia mfano wa riadha iliyofanyika kule Qatar, mwaka huu, ambako Tanzania tuliambulia patupu licha ya kwamba wanariadha wetu ni mahiri na wanazo rekodi zilizotukuka duniani, lakini kilichokuja kusemwa ni kuwa hakukuwa na maandalizi mazuri ndani ya Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), na kwamba kila mmoja alijifanyia mazoezi kivyake.

Ipo michezo mbalimbali ilifanyika kule Morocco, ile ya Afrika, ambayo pia timu zetu zilitia aibu kwa kurejea kama wasindikizaji. Yote haya ni ama maandalizi mabovu au migogoro ndani ya vyama husika ilichangia hali kutokuwa hali na kuchangia kuathiri matokeo.

Wakati masuala ya migogoro ndani ya vyama sio mada yetu leo, kwa leo tutazungumzia hali ya mambo ndani ya klabu ya Yanga, yenye umri wa zaidi ya miaka 80 sasa, ambako Kocha Mkuu, Mwinyi Zahera na benchi lake la ufundi wameondolewa baada ya wakubwa kutoridhishwa na hali ya mambo.

Kwanza kabisa tunawapa pole walioguswa na uamuzi huo kinyume na jinsi walivyotarajia. Tunaamini kwamba kila jambo lina wakati wake na huu ni wakati sahihi uliofika kwa uongozi wa klabu hiyo kuchukua uamuzi ili mambo yaweze kuendelea kama wanavyotaka, ikizingatiwa kwamba timu ndiyo huwapa furaha mashabiki. Hivyo wasipofurahi ina maana kuna mahali hapaendi vizuri.

Kwa Yanga iliyosota kwa misimu miwili ikipitia kipindi kigumu, ikiwamo kutembeza bakuli ili mambo yaende inapaswa kufanya mambo kadhaa baada ya kuachana na akina Zahera, kubwa ikilenga katika utulivu ambao utachagizwa na matokeo mazuri uwanjani na si vinginevyo.

Mosi, tunauomba uongozi wa klabu hiyo ufanye tathmini pana ili kusaidia benchi jipya la ufundi kufanya vizuri uwanjani. Tunasema hivyo kwa sababu tunaamini kwamba huenda wamechukua uamuzi wa kuachana na makocha wao kumbe kuna mahala panapovuja na hivyo panafaa kuzibwa. Hili tunalisema tukirejea kauli ya kocha huyo aliyeondolewa ambaye amewatuhumu baadhi ya viongozi kutoitendea haki klabu, ikiwemo katika masuala yanayohusiana na fedha ambapo kuna nyakati, kwa mujibu wa Zahera, wahusika walikuwa wakibana fedha hata zilizopaswa kulipia chakula cha wachezaji hadi alipoamua kuzama mfumoni mwake kunusu hali ilhali fungu lilikuwa mikononi mwa viongozi walioambatana na timu.

Kwa hili iwapo itathibitika kuwa ni kweli, basi viongozi wachukuliane hatua wao kwa wao ili mwisho wa siku hali hii isijirudie tena. Hii ni kwa sababu iwapo itaachwa iendelee kuwepo hata likija benchi jipya la ufundi la kudumu litakumbana na kadhia hiyo. Jambo jingine ni mfumo. Inavyoonekana kuna mahali katika mfumo au falsafa ya Yanga panakosewa. Hivi kwanini tangu alipoondoka Maji na watu wake mambo hayabadiliki? Ni vyema viongozi wakae chini watafakari namna ya kuja na mfumo utakaoendana na falsafa ya timu hiyo kongwe nchini.

Hatutegemei kuona kila mara Wanayanga wakiumia kwa mambo yaliyo ndani ya uwezo wa kimfumo na falsafa ya timu yao. Yanga ni timu kubwa inastahili kubakia kuwa hivyo hata kama itakuwa inapita katika mabonde na kupanda milima.

La tatu, uwepo wa mtu anayekaimu katika suala la utendaji kwa kipindi kirefu si jambo zuri hasa kwa taasisi kubwa yenye mashabiki lukuki kama Yanga. Ni katika hali hiyo mtu anaweza kuhusisha hata hali ya sintofahamu inayoiandamana na kutokuwa na mtendaji wa kudumu muda mrefu.

Ni vyema uongozi wa Dk Mshindo Msolla ukafanya uamuzi ambao utaipa klabu mtendaji wa kudumu ili aweze kuweka mambo sawa.

Tunaposema hili hatuna maana kwamba aliyepo hafai, la hasha, inawezekana anafaa lakini kwa kufanya akikaimu nafasi hiyo huenda kuna mambo anashindwa kuyafanyia uamuzi akichelea kuondolewa. Si hivyo tu, lakini huenda kuna mambo ambayo kwa kukaimu kwake hapaswi kuyagusa.