Vikwazo anavyopaswa kuvivuka Mbwana Samatta ili kuichezea Aston Villa

Muktasari:

Wakati ada ya usajili huo ikiripotiwa kukubaliwa, Samatta bado hajasaini maslahi binafsi huko Villa, na hii ni taratibu za kawaida japo kuna kikwazo kingine kama kinachowakabili wachezaji wengine wa Villa kama Marvelous Nakamba na Douglas Luiz, ambapo naye Samatta anatakiwa kupata kibali cha kazi Uingereza ili kuweza kucheza soka nchini humo.

Dar es Salaam. Ripoti kutoka nchini Ubelgiji zimeeleza kuwa klabu ya soka ya Aston Villa imepanga kutumia Pauni 8.5 milioni kumsajili mshambuliaji Mbwana Samatta kutoka klabu ya RC Genk inayoshiriki Ligi Kuu ya Ubelgiji (Jupiler Pro League).

Katika msimu huu, Mbwana Samatta ameifungia klabu hiyo ya Genk mabao 10 katika Ligi Kuu ya soka nchini Ubelgiji na anatarajiwa kuwa mbadala wa mshambuliaji Wesley ambaye amepata majeraha ya goti yatakayomuweka nje hadi mwishoni mwa msimu.

Wakati ada ya usajili huo ikiripotiwa kukubaliwa, Samatta bado hajasaini maslahi binafsi huko Villa, na hii ni taratibu za kawaida japo kuna kikwazo kingine kama kinachowakabili wachezaji wengine wa Villa kama Marvelous Nakamba na Douglas Luiz, ambapo naye Samatta anatakiwa kupata kibali cha kazi Uingereza ili kuweza kucheza soka nchini humo.

Hii ina maana kuwa hata kama dili hilo likisainiwa na Samatta ndani ya saa 24, bado mshambuliaji huyo hataweza kuicheza klabu ya Villa dhidi ya Brighton kesho Jumamosi.

Mshambuliaji huyo ameishi na kufanya kazi kwa muda mrefu nchini Ubelgiji tangu mwaka 2016, hivyo kuna uwezekano kuwa alishaomba uraia wa Ubelgiji na pasipoti ya Umoja wa Ulaya japo madai hayo hayajathibitishwa bado na kitu kingine Tanzania hawaruhusu uraia wa nchi mbili na nyongeza ni kwamba itakuwa ngumu kwa Samatta kupata pasipoti hiyo kutokana na kuichezea timu ya Taifa ya Tanzania.

Mshambuliaji huyo amekuwa akifurahia maisha yake huko Ulaya lakini kama uhamisho wake kwenda England utakubaliwa Samatta atatakiwa kupitia sheria kali zinazotumika kwa wanasoka wasiotoka kwenye nchi za Ulaya na ambao hawana pasipoti za nchi zilizo katika Umoja wa Ulaya.

Kwakuwa Tanzania haipo katika umoja wa nchi hizo za Ulaya Samatta atahitaji kibali cha kuweza kufanya kazi nchini Uingereza.

Suala la namna gani mshambuliaji huyo atapata kibali cha kazi, Shirikisho la Soka linatumia mfumo wa pointi na klabu inatakiwa kuomba kupitia shirikisho hilo, ambapo wakati mwingine kunakuwa na kuondolewa kikwazo hicho na kupewa kibali licha ya kutokuwa na pointi zinazotakiwa.

Suala la kupitia mfumo wa pointi linawezesha kupata kibali hicho lakini hii hutokea endapo mchezaji ambaye ni mkubwa na wa kimataifa ambaye nchi yake ipo katika nafasi ya kumi katika viwango vya ubora wa soka vya shirikisho la soka la kimataifa (Fifa), ambapo hadi sasa Tanzania haijafika kiwango hicho.

Mara ya mwisho, Tanzania kushika nafasi ya 70 katika viwango vya ubora vya soka vya Fifa ilikuwa ni mwaka 1995, lakini hivi sasa nchi hiyo inashikilia nafasi ya 134 hii inaashiria kuwa Samatta anatakiwa kukusanya pointi za kutosha kupitia vigezo mbalimbali.

Miongoni mwa vigezo ambavyo Samatta anaweza kupata pointi ni kupitia kucheza mechi nyingi kwenye timu aliyopo hivi sasa ya Genk, kupata pointi kwa kucheza mashindano ya Ulaya, na ya kimataifa akiwa na timu ya Taifa. Aidha pia mshambuliaji huyo ataweza kupata pointi kupitia ada ya uhamisho.

Lolote linaweza kutokea kuanzia sasa kwani Samatta amecheza timu hiyo muda mrefu kwa mafanikio makubwa, lakini pia amecheza mashindano kama UEFA na Europa huku akicheza mashindano mbalimbali akiwa na kikosi cha timu ya Taifa Tanzania.