Vijeba AFCON waitisha Serengeti

Muktasari:

 

  • Tanzania na Angola ndiyo tunaonekana kuwa na wachezaji wenye maumbo madogo

Dar es Salaam. Maumbo na miili mikubwa ya wapinzani wa Serengeti Boys kwenye fainali za Afrika kwa vijana (Afcon U 17) yamemshtua kocha wa timu hiyo, Oscar Mirambo ambaye amesema,  ameanza kuwajenga vijana wake ili kuwaondolea hofu ya maumbo ya wapinzani wakati wa mashindano.

Serengeti Boys iko kundi A na Angola, Nigeria na Uganda huku kundi B ina timu za cameroon, senegal, Morocco na Guinea katika fainali hizo zitakazoanza Aprili 14 hadi 29 jijini Dar es Salaam.

Mirambo anasema katika timu hizo nane zinazowania nafasi ya kucheza kombe la dunia la vijana, timu sita zina wachezaji wenye maumbo makubwa.

"Tanzania na Angola ndiyo tunaonekana kuwa na wachezaji wenye maumbo madogo, lakini timu nyingine zilizosalia wachezaji wao wote wana miili na maumbo makubwa," anasema Mirambo.

Alisema katika mpira umbo la mchezaji ni 'advantage' ukiachana na kipaji, lakini ameanza kuwajenga wachezaji ni namna gani wanapaswa kucheza wanapokutana na wachezaji wenye maumbo makubwa.

"Katika soka kuna umbo na kipaji, wachezaji wangu wana maumbo madogo, lakini wana vipaji, wenzetu wana bahati ya maumbo makubwa, inaweza kuwa changamoto, lakini tunajijenga ili kuweza kuwadhibiti wachezaji wa aina hiyo.

Akizungumzia maandalizi ya kikosi chao, Oscar amesema timu ina morali ya ari ya juu na wakati wowote kuanzia Kesho Jumatano wataondoka nchini kuelekea Dubai kwenye kambi yao ya mwisho kuelekea kwenye mashindano.